WAKATI duru la kwanza katika Ligi Kuu Zanzibar likimalizika, mambo mbalimbali yamejitokeza ikiwamo kufungiwa kwa waamuzi, wachezaji, viongozi na hata mashabiki walioonekana kwenda kinyume cha utaratibu.
Mwanaspoti linakuchambulia mambo sita yaliyojiri katika duru hilo la kwanza la Ligi Kuu Zanzibar inayoshirikisha timu 16.
RUNGU LA WAAMUZI
Waamuzi sita wa ligi hiyo wamekutana na adhabu ya kufungiwa kuchezesha baadhi ya mechi, kati yao mwamuzi mmoja ameondolewa kwenye ratiba hiyo kwa kushindwa kuzitafsiri na kuzisimamia sheria za mpira wa miguu.
Waamuzi waliokutana na adhabu hiyo ya kufungiwa ni Yunus Kombo, Washington Benard, Thobias Wariko, Is-haka Yona, Saleh Mohamed na Fikirini Juma.
Fikirini amepigwa rungu la kuondolewa kwenye ratiba ya waamuzi watakaochezesha kwa michezo yote iliyosalia msimu wa 2025-2026.
Kikao kilichofanywa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Novemba 5, 2025, kilimuondoa Mwamuzi Fikirini kwenye ratiba ya waamuzi watakaochezesha michezo iliyosalia msimu huu.
Katika hatua nyingine, Bodi hiyo ilimuondoa mwamuzi Benard kwenye ratiba kwa mizunguko mitano baada ya kushindwa kuzitafsiri na kuzisimamia sheria katika mchezo uliochezwa Oktoba Mosi, kati ya JKU na KVZ, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku timu ya JKU ikipata bao la tatu lililokataliwa na mwamuzi huyo ikidaiwa mfungaji aliotea.
Mwamuzi Thobias Wariko amefungiwa miezi sita kuchezesha mchezo wowote unaondaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) na faini ya Sh500,000 kwa kutozingatia sheria katika mechi ya Mafunzo dhidi ya Malindi, iliyochezwa Novemba 13, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A.
Kabla ya kufungiwa, Kamati ilimpa onyo kali na kumtaka awe makini wakati wote wa mchezo baada ya kuonekana kuna sheria za mpira wa miguu ameshindwa kuzitafsiri.
Pia, Kamati ilimfungia kwa miezi mitatu na faini ya Sh500,000, mwamuzi wa mchezo wa Mwembe Makumbi dhidi ya KVZ, Yunus Kombo uliochezwa Novemba 14, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A.
Waamuzi I-shaka Yona Thomas na Msaidizi wake Saleh Khalfan Mohamed wamefungiwa miezi mitatu na kutozwa faini ya Sh500,000 kila mmoja katika mechi ya Chipukizi dhidi ya New Stone, iliyochezwa Novemba 9, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba.
TIMU KUTOZWA FAINI
Junguni United imekuwa timu ya kwanza msimu huu kutozwa faini ya Sh200,000 kwa kufika uwanjani bila ya kuvaa jezi jambo ambalo lilisababisha kuvunjwa kwa mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa Septemba 26, 2025 kati ya Junguni na Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba.
Katika kikao cha kamati ya Bodi, mzunguko wa 3, 4, Kamati hiyo iliitoza faini ya Sh1 milioni timu ya Polisi kwa kumtumia mtu ambaye hakuorodheshwa kuingia uwanjani kusimamia mazoezi ya viungo ya wachezaji na mchezaji wa timu huyo kwenda kwenye goli la Mlandege na kurusha vitu mithili ya mchanga, kitendo kinachoshabihiana na imani za kishirikina.
Vilevile, Bodi ya Ligi Zanzibar imezitoza faini ya Sh1 milioni timu mbili ikiwamo Mlandege na Mwembe Makumbi kwa kosa la kuvaa jezi ambazo hazina mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Zanzibar (PBZ).
Timu ya Kipanga ilitozwa faini ya Sh500,000 kwa kutumia mlango wa upande wa Mashariki mwa Uwanja wa Mao, ambao sio rasmi kutumika na klabu.
Timu ya Mlandege imetozwa faini hiyo kuvaa jezi ambazo hazina nembo ya mdhamini wa ligi katika mchezo dhidi ya KMKM, kitendo ambacho ni kinyume cha kanuni ya tatu za mashindano ya ligi 2025-2026 na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa sura ya 26 na Mwembe Makumbi imekumbana na adhabu hiyo katika mchezo wake wa Uhamiaji.
MUEMBE MAKUMBI KUCHEZA BILA MASHABIKI
Timu hiyo ilifungiwa kuingiza mashabiki wake katika michezo minne mfululizo na kutozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la kufanya vurugu wakati wa mchezo dhidi ya KVZ na kulipa gharama za uharibifu wa miundombinu ya uwanja.
ADHABU KWA VIONGOZI, WACHEZAJI
Meneja wa timu ya Muembe Makumbi, Salum Salum, alizuiwa kukaa kwenye benchi la ufundi kwa miezi mitatu mfululizo, huku shabiki wa timu hiyo, Omary Othman ‘Gago’ akitozwa faini ya Sh500,000 na kufungiwa kutazama mchezo wowote wa ZFF kwa miaka miwili.
Pia, mchezaji wa timu hiyo, Salum Ali Mlingo alifungiwa michezo mitano ya Ligi Kuu kwa kuonyesha mchezo usio wa kiungwana kwa kumchezea rafu mchezaji wa KVZ, Majid Bakari na kulimwa kadi nyekundu.
Kamati ya Uendeshaji ilimfungia Kocha Msaidizi wa KVZ, Hassan Makame Ameir kwa miezi mitatu na faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumsukuma mwamuzi msaidizi wakati wa vurugu dhidi ya Muembe Makumbi.
Naye, kiongozi wa KVZ, Hassan Chura alipewa onyo kwa kosa la kuingia uwanjani kinyume cha utaratibu wakati wa mchezo.
Vilevile, Bodi hiyo ilimfungia mchezaji wa timu hiyo, Kassim Ame kwa kosa la kuonyesha mchezo usio wa kiungwana.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Malindi, Namala Suleiman alipewa onyo kwa kutoa maneno yasiyofaa kwa waamuzi wakati timu hiyo ilipocheza dhidi ya Mafunzo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo kumalizika.
Naye, Khalfan Ngasa, shabiki wa timu hiyo alifungiwa kutazama mechi tatu mfululizo kwa kosa la kutoa lugha chafu mbele ya waandishi wa habari wakati wakitekeleza majukumu yao.
NEW STONE INATESEKA
Kati ya timu nne zilizopanda daraja msimu huu kutokea Pemba, New Stone haijavuna alama hata moja tangu kuanza kwa Ligi.
Nyavu za timu hiyo zimetikiswa mara 39 ikifuatiwa na Junguni iliyofungwa mabao 20 katika michezo 12, New Stone haijafanikiwa kushinda mechi yoyote na kufunga mabao sita tu tangu kuanza kwa msimu na inashikilia nafasi ya mwisho katika msimamo wa PBZ.
Fufuni ni kati ya timu nne zilizopanda daraja na kufanya vizuri katika Ligi hiyo na ipo nafasi ya pili ya msimamo wa ZPL.
Katika mechi 15 ambazo imeshacheza timu hiyo imeshinda tisa, imetoa sare tatu na imepoteza tatu huku ikivuna pointi 30. Timu hiyo ilijenga heshima ya utawala wake baada ya kuitandika KVZ bao 1-0, kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.
Mafunzo inashikilia rekodi ya kutoa sare mechi nane kati ya 15 ilizocheza ikifuatiwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Mlandege waliotoa sare sita wakifuatiwa na Malindi na JKU zenye sare tano.
Uhamiaji ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi katika msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na mabao 29 katika mechi 15 na kufungwa mabao 13.