
Esperance ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa nchini Burundi alikokimbilia kufuatia mapigano mashariki mwa taifa hilo la Maziwa Makuu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limefikisha kilio hicho kwa wadau na sasa Japan imelipatia dola Laki Sita na Elfu Ishirini na Tano kwa ajili ya usaidizi wa chakula cha kuokoa maisha kwa wakimbizi hao na wale wa Burundi waliorejea kutoka Tanzania.
WFP kupitia taarifa yake inasema mwezi uliopita wa Desemba ilipokea wakimbizi 85,000 kutoka DRC na imeimarisha usaidizi wa vyakula vilivyopikwa na vikavu kwa wakimbizi wapya 80,000.
Mwakilishi Mkazi wa WFP nchini Burundi Jean-Noel Gentile anasema msaada wa fedha kutoka Japan umekuja wakati muafaka kwa familia zinazokimbia ukosefu wa usalama na wale wanaorejea kutoka ukimbizini Tanzania bila kitu chochote.
Msaada huo utawezesha WFP kwa kushirikiana na serikali ya Burundi, kusambaza msaada wa chakula cha kuokoa maisha na kulinda utu wa binadamu wakati wa dharura hii.
Kutokana na mipango ya kufunga kambi za wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania, ifikapo katikati ya mwaka huu wa 2026, warundi wapatao 93,000 wanatarajiwa pia kurejea Burundi na kuweka shinikizo la mahitaji.
Kwa sasa wakimbizi 1,500 hurejea Burundi kila wiki na yakadiriwa idadi inaweza kuongezeka hadi 3,000 kwa wiki.