Gazeti la The Wall Street Journal limeandika katika ripoti yake kwamba: “Marekani imepoteza hadhi yake ya kimataifa kwa kiasi kikubwa katika miaka 25 ya kwanza ya karne ya 21, kutokana na utawala mbaya, vita vya gharama kubwa na migogoro ya ndani.”
Katika ripoti ya kiuchambuzi, The Wall Street Journal limechunguza miaka 25 ya kwanza ya karne ya 21 nchini Marekani na kutaja kipindi hicho kuwa wakati wa kupungua polepole nguvu ya taifa la Marekani. Kwa mujibu wa chombo hicho cha habari, mwishoni mwa karne ya 20, Marekani ilikuwa katika kilele cha nguvu za kiuchumi, kijeshi na kisiasa; mapato yalikuwa yakiongezeka, Serikali ya Shirikisho ilikuwa na ziada ya bajeti kwa miaka kadhaa mfululizo na ushirikiano wa vyama viwili uliwezesha maamuzi muhimu kufanywa. Lakini karne ya 21 ilipoanza, mkondo wa nchi ulibadilika.
Mojawapo ya mambo yaliyosababisha mabadiliko hayo ni uungaji mkono wa vyama viwili vikuu (Democratic na Republican) kwa China kujiunga na Shirika la Biashara Duniani, hatua iliyowezesha kuingia kwa wingi bidhaa za bei nafuu na kusababisha kupotea sehemu kubwa ya ajira katika sekta ya uzalishaji nchini Marekani. Mchakato huu ulipunguza viwango vya maisha ya wafanyakazi wengi na kuandaa mazingira ya kutoridhika kijamii.
Mashambulizi ya Septemba 11, 2001 pia yalibadilisha mwelekeo wa sera za kigeni za Marekani. Utawala wa George W. Bush ulianzisha vita vya muda mrefu nchini Afghanistan na Iraq ambavyo vilipelekea kughafilika na ustawi na maendeleo ya kasi kubwa ya China. Mbali na gharama zake kubwa, vita hivyo pia vilidhoofisha uungaji mkono wa umma kwa ushirikiano wa kimataifa nchini nchini Marekani.

Katika upande mwingine, hali ya kifedha ya Marekani ilizorota kwa kasi. Utabiri wa kupatikana ziada kubwa ya bajeti mwanzoni mwa miaka ya 2000 haukutimia, na kupungua kodi na ongezeko la matumizi vilizidisha deni la taifa.
Hatimaye, usimamizi mbaya wa janga la COVID-19 ulizidi kupunguza imani ya umma kwa taasisi za serikali ya Marekani.
Gazeti la Wall Street Journal hatimaye linaangazia matatizo mbalimbali ya Marekani ikiwa ni pamoja na mgogoro wa nyumba na idadi kubwa ya watu wazee, (kuzeeka jamii) mashinikizo kwenye programu za kijamii, kudhoofisha imani ya washirika kwa Marekani na kuimarika kijeshi nchi ya China, na kusisitiza kwamba kutokana na mashinikizo hayo yanayoongezeka, viongozi wa kisiasa wa Marekani wanalazimika kushughulikia kwa ujasiri matatizo ya msingi ili kukomesha miaka 25 ya kudorora na kuanza njia ya ukarabati.