Mawaziri wa Mambo ya Nje wa mataifa manane ya Waislamu wameitaka jamii ya kimataifa kuishinikiza Israel, kama dola linalokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, kuondoa mara moja vizingiti na vikwazo vya kuingia kwa misaada ya msingi na ya dharura katika Ukanda wa Gaza.

Wanadiplomasia hao wakuu kutoka Ufalme wa Saudi Arabia, Ufalme wa Kihashim wa Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jamhuri ya Indonesia, Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan, Jamhuri ya Uturuki, Taifa la Qatar, na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri walitoa mwito huo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Ijumaa.

Mawaziri hao wameitaka jamii ya kimataifa “kutekeleza majukumu yake ya kisheria na kimaadili na kuishinikiza Israel, kama mamlaka inayokalia kwa mabavu (ardhi za Wapalestina), kuondoa mara moja vikwazo vya kuingia (Gaza) na usambazaji wa vifaa muhimu, ikiwa ni pamoja na mahema, vifaa vya makazi, msaada wa kimatibabu, maji safi, mafuta, na usaidizi wa usafi wa mazingira.”

Wamesisitiza kwamba, hali mbaya ya hewa imeshadidisha hali ya kibinadamu iliyopo katika eneo hilo lililozingirwa, hasa kwa karibu watu milioni 1.9 na familia zilizohamishwa kwenye makazi yao, sasa zimebanana katika makazi machache.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alilaani marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, Knesset Desemba 29, yanayohusu kusitishwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), pamoja na mashirika mengine 30. Katibu Mkuu wa UN amesema,  marekebisho hayo yanalenga kuzidisha kuzuia uwezo wa UNRWA kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake yaliyoidhinishwa. 

Wizara ya utawala wa Kizayuni inayohusika na masuala ya Diaspora imedai kuwa mashirika hayo yameshindwa kufungamana na sheria mpya za usajili zinazojumuisha kukaguliwa wafanyakazi na kuwasilisha taarifa za mtu binafsi kwa ajili ya kuajiriwa. 

Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Makanisa Duniani (WCC) limeutaka Umoja wa Ulaya (EU) kuiwekea Israel vikwazo vikiwemo vya silaha kutokana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza, na ukiukaji wa haki dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *