
Kama ilivyo ada, Mwakilishi wa Kudumu wa taifa linalochukua usukani wa Baraza la Usalama huzungumza na waandishi wa habari kuelezea programu ya mwezi mzima na vivyo hivyo kwa Mwakilishi wa Kudumu wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Abukar Dahir Osman.
Kaitka mazungumzo yake leo Januari 02 aliwaeleza waandishi wa habari programu yake lakini vile vile alijibu maswali ya waandishi wa habari ikiwemo la Israeli kuitambua Somaliland kama taifa huru na lenye mamlaka.
Amesema kitendo hicho, “ni juhudi ya makusudi ya nguvu ya Israeli inayokalia maeneo ya wengine ili kuugeuza mwelekeo wa dunia,” na akasema kuwa taarifa zinazodai kuwa Somaliland “ilikubali kwa siri” kupokea wapalestina milioni 1.5 wanaotarajiwa kuhamishwa huko kutoka Gaza zingekuwa “hazikubaliki.”
Balozi wa Somalia ameshukuru wajumbe wa Baraza la Usalama ambao mapema wiki hii kwa kauli moja waliunga mkono “uhuru wa mamlaka na uadilifu wa eneo la Somalia.”
Bendera za nchi 5 zinazoingia Baraza la Usalama zapandishwa
Mwaka mpya wa 2026 ukianza, vivyo hivyo kwa wajumbe wapya 5 wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao ni Bahrain, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), Latvia na Liberia.
Ujumbe wao utakuwa wa miaka miwili baada ya mataifa mengine 5 ambayo ni Algeria, Guyana, Korea Kusini, Sierra Leone na Slovenia, kumaliza ujumbe wao wa miaka miwili mwezi Desemba mwaka jana.
Hafla ya kupandisha bendera za nchi hizo tano kwenye eneo la ukumbi wa Baraza la Usalama imefanyika mchana wa leo Januari 02, 2026 ambapo ni mara ya kwanza kwa Latvia kuwa na ujumbe wa Baraza la Usalama.
Kauli za DRC na Latvia
Noëlla Ayeganagato Nakwipone, ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC amezungumza baada ya hafla hiyo na kusema kuwa, “kuhusu amani na usalama, tutachangia kwa kina kwenye mijadala ya Umoja wa Mataifa kuhusu mustakabali wa operesheni za Umoja wa Mataifa za ulinzi wa amani. Kama mwenyeji wa misheni kubwa zaidi ya ulinzi wa amani kwa zaidi ya miongo miwili, DRC ina uzoefu wa kina kuhusu changamoto na vikwazo vya mbinu hizi.”
Kwa Latvia, Mwakilishi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Sanita Pavļuta-Deslandes amesema “uwepo wetu kwenye Baraza la Usalama unaakisi safari yetu ndefu kutoka magumu hadi ustawi, kutoka matamanio hadi mchango thabiti. Tunaamini ushiriki wajibifu wa taifa, liwe dogo au kubwa unaimarisha amani na usalama duniani.”
Je nchi hizo 5 zinachukua nafasi za nani ?
Nchi 5 zinazoingia mwaka huu zinaungana na nyingine 5 zisizo na ujumbe wa kudumu ambazo ni Denmark, Ugiriki, Pakistan, Panama na Somalia – ambazo ujumbe wao utakoma mwishoni mwa mwaka huu wa 2026.
Kwa kuwa Baraza la Usalama lina wajumbe 15, wajumbe 5 waliosalia wana ujumbe wa kudumu na kura turufu na hujulikana kama _5 nao ni Ufaransa, China, Urusi, Uingereza na Marekani.
Kura turufu ya nchi yoyote kati ya hizo P5 ina uwezo wa kuzuia hoja yoyote inayopigiwa kura hata kama iwe imepata kura nyingi.
Soma udadavuzi kwa lugha ya kiingereza hapa.