
Kaimu Rais wa Venezuela, aliyeidhinishwa na Mahakama ya Juu Zaidi nchini humo, amesema kulikuwa na “kivuli cha Wazayuni” katika operesheni ya kutekwa nyara Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro.
Rodríguez, ambaye aliteuliwa kama kiongozi wa muda wa Venezuela amesema kwamba, Maduro na mkewe, ambao walisafirishwa na kuwekwa kizuizini huko New York baada ya kutekwa nyara, wanapasa kuavhiwa huru mara moja. Katika hotuba ya televisheni Jumamosi usiku, kiongozi huyo amelaani shambulio hilo la majeshi ya Marekani, akisema kuwa lilikuwa na “mkono wa Kizayuni.”
Baada ya vikosi vya Marekani kushambulia Caracas mapema Jumamosi, na kutekwa nyara kwa Maduro, Mahakama ya Juu ya Venezuela ilimteua Makamu wa Rais, Delcy Rodríguez kama rais wa muda ili kuhakikisha kuwa hakuna ombwe la uongozi na kuunda Baraza la Ulinzi la Taifa la nchi hiyo.
Wakati wa hotuba yake hiyo jana, Rais wa muda wa Venezuela alisisitiza kwamba, Maduro anasalia kuwa “rais pekee wa Venezuela” na akataka kuachiliwa kwake mara moja.
Rodríguez alielezea shambulio hilo kama “uchokozi wa kijeshi usio na kifani” wa Marekani, akisisitiza kwamba lilichochewa na nia ya kunyakua udhibiti wa hifadhi kubwa ya mafuta ya Venezuela.
Rodríguez amebainisha kwamba, serikali nyingi duniani kote zimeshangazwa na uvamizi huo wa Marekani dhidi ya taifa hilo la Amerika ya Latini, akisisitiza kwamba “historia na haki vitawafanya walipe gharama kubwa (kwa hatua yao).”