Hatua ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na kutekwa nyara Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, imekabiliwa na wimbi kubwa la laana na ukosoaji mkubwa kote duniani.

Nchi nyingi zimelaani kitendo hicho, na taasisi nyingi za kimataifa zimeitaja hatua hiyo ya Trump kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na zimetoa wito wa kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa ya nchi zote na kubuniwa utatuzi wa amani wa mgogoro wa Venezuela. Serikali ya Venezuela imeitaja hatua hiyo kuwa ni “uvamizi wa kijeshi” na, kutangaza hali ya hatari kote nchini humo. Vilevile imeitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kadhia hiyo.

Kwa kuishambulia Venezuela, Marekani imeonyesha tena kwamba sheria za kimataifa na kanuni za msingi za mamlaka ya nchi huru havina nafasi yoyote katika mantiki na kamusi yake ya kisiasa. Shambulio la kijeshi na kuteka nyara rais wa nchi huru si tu kwamba haviwezi kuhalalishwa na kutetewa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, lakini pia, kama uzushi hatari, vihatarisha nidhamu ya kimataifa. Wakati huo huo, nafasi na mchango wa Donald Trump kama mbunifu na mtekelezaji wa sera hiyo ni muhimu; kwani tabia yake ya kujichukilia maamuzi ya upande mmoja, imegeuza sera ya kigeni ya Marekani kuwa uwanja wa maonyesho ya kutunisha misuli na utumiaji mabavu usio na mantiki ambao sasa umekasirisha nchi nyingi kote duniani, hata washirika wa Washington.

Shambulio la Marekani dhidi ya Venezuela linaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kutokana na matokeo yake makubwa katika ngazi za kikanda na kimataifa.

Katika ngazi ya kisheria, hatua ya Marekani ni ukiukaji wa wazi wa kanuni ya kutoingilia kati masuala ya nchi huru na marufuku ya matumizi ya nguvu.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa unakataza waziwazi tishio au matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya ardhi na mamlaka ya kisiasa ya nchi inayojitawala. Kumteka nyara rais wa nchi huru na kumhamishia kwenye ardhi ya Marekani kuna maana ya kupuuza uhuru wa mahakama na taasisi za kisiasa za Venezuela. Kitendo hiki ni sehemu hatari zaidi ya kadhia hii. Kwani iwapo mtindo kama huo utaruhusiwa, mzozo na hitilafu yoyote ya kisiasa duniani inaweza kumalizika kwa kukamatwa rais wa nchi kwa kutumia kisingizio chochote cha masuala ya usalama.

Wasiwasi huu ndio unaozifanya nchi na maoni ya umma kulaani uvamizi wa Marekani huko Venezuela, kwa sababu kuvunjwa mipaka hiyo kunatishia usalama wa nchi zote, na kama alivyosema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, “hakuna nchi yenye haki ya kumkamata kiongozi wa taifa huru. Kitendo hiki ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na tishio kwa usalama wa pamoja.” Matamshi haya yanaonyesha kwamba upinzani wa kimataifa dhidi ya kitendo cha Marekani si tu kutokana na mtazamo wa kisiasa, bali pia kwa kuzingatia mtazamo wa kisheria na kanuni za msingi za nidhamu ya kimataifa.

Katika upande wa kihistoria na kisiasa, hatua ya Marekani huko Venezuela inakumbusha “Mwongozo wa Monroe” (the Monroe Doctrine) na uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya nchi za Amerika ya Kusini. Kumbukumbu ya pamoja ya eneo la Amerika Kusini imejaa mifano ya uingiliaji kati wa Marekani ulioanza kwa kaulimbiu ya kulinda nidhamu na usalama, na kuishia kwenye majeraha makubwa kwa uhuru na jamii. Katika muktadha huu, tunaweza kuashiria mfululizo wa mapinduzi na uvamizi wa Marekani katika nchi za Amerika Kusini, kwani eneo hilo limekuwa mwathirika wa mara kwa mara wa sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Washington. Akizungumzia tukio hili, Rais wa zamani wa Ecuador, Rafael Correa amesema: “Kitendo hiki cha Marekani kinakumbusha siku zenye giza zaidi za uvamizi wa kijeshi Amerika Kusini. Iwapo jamii ya kimataifa haitasimama, kesho itakuwa zamu ya nchi nyingine.”

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ambaye siku ya Jumamosi (03.01.2026) alitekwa nyara na Marekani

Katika ngazi ya kiuchumi, Venezuela, ikiwa moja ya wamiliki wa akiba kubwa ya mafuta duniani, ina nafasi isiyo na kifani katika mlinganyo wa nishati wa kimataifa.

Kwa akiba yake kubwa ya mafuta ghafi, nchi hiyo imekuwa ikikodolewa macho na mataifa makubwa, kwa sababu mabadiliko yoyote katika hali yake ya kisiasa na kiuchumi yanaweza kuathiri usambazaji na mahitaji ya mafuta duniani.

Katika muktadha huu, Trump kwa muda mrefu sasa, amekuwa na ndoto ya kutia mkononi rasilimali za mafuta za Venezuela na amezungumzia mara kwa mara umuhimu wa akiba hiyo katika hotuba zake. Sasa, mara tu baada ya uvamizi kijeshi dhidi ya Caracas, Rais wa Marekani amezungumza waziwazi kuhusu kupelekwa kampuni kubwa zaidi za mafuta za Marekani nchini Venezuela na ameahidi kwamba kampuni hizo zitawekeza mabilioni ya dola katika sekta ya mafuta ya nchi hiyo. Taarifa hizi zinaonyesha kwamba nyuma ya hatua ya masuala ya kijeshi kuna nia ya kiuchumi na utajiri wa nishati; nia hiyo inalenga kupanga upya soko la mafuta kwa maslahi ya Washington na washirika wake.

Kwa mtazamo wa kisiasa, hatua hiyo ya Marekani imetilia shaka sana uhalali wa nchi hiyo kimataifa. Washirika wa jadi wa Washington barani Ulaya pia wamelaani hatua hiyo.  Kaja Kallas, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema: Katika hali yoyote ile, kanuni za sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa lazima ziheshimiwe.” Msimamo huu unaonyesha kwamba hata washirika wa karibu wa Marekani hawataki kukubali sera kama hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *