
Ni wachache wanaoweza kufikiria kupona katika ajali ya gari ya kusikitisha iliyogharimu maisha ya marafiki wawili wa karibu. Lakini kwa Anthony Oluwafemi Olaseni Joshua, tukio hilo lilikuwa na uchungu wa ziada kwa kuwa lilitokea nchini Nigeria, ardhi ya wazazi wake na asili ya familia yake.
Joshua ambaye aliokolewa kwenye ajali hiyo na wasamaria wema, aliumia na kupelekwa hospitali ambapo juzi alitoka hospitalini na kwenda machwari moja kwa moja sehemu walipo rafiki zake ambao walifariki kwenye ajali hiyo.
Joshua, aliyezaliwa Uingereza lakini mwenye asili ya Nigeria na Ireland kupitia wazazi wake Robert na Yeta, alikuwa amerudi Nigeria kwa furaha kubwa baada ya ushindi wake mzito dhidi ya Jake Paul, uliomuingizia kiasi kikubwa cha fedha kinachokadiriwa kufikia pauni milioni 70 zaidi ya shilingi 160 bilioni.
Badala ya kutumia utajiri huo katika maeneo ya kifahari kama wanavyofanya wanamichezo wengine maarufu, Joshua alichagua kurejea katika ardhi ya mababu zake, Jimbo la Ogun, kusherehekea mafanikio yake na familia pamoja na marafiki wa karibu.
Katika historia, Joshua amepigana mapambano 29 ameshinda kwa knockout mapambano 26, amepoteza mapambano manne, baadhi ya watu maarufu ambao wamewahi kupigana na Joshua ni Jake Paul, Daniel Dubois, Francis Ngannou, Oleksandr Usyk pamoja na Jermaine Franklin.
Safari hiyo ya gari
Nigeria imekuwa sehemu muhimu ya safari ya maisha na taaluma ya Anthony Joshua, naye kwa upande wake amekuwa mmoja wa wana waliopendwa sana na taifa hilo. Takribani mwaka mmoja uliopita, Joshua alikuwa mgeni wa heshima katika makazi ya Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ambapo alimkabidhi glavu ya ndondi iliyosainiwa. Rais Tinubu alimuelezea Joshua kama “bingwa wa kweli na balozi anayestahili wa Nigeria.” Mwaka mmoja baadaye, rais huyo huyo alizungumza naye akiwa amelazwa hospitalini baada ya kuungua.
Uridhi wa kifalme
Asili ya Joshua nchini Nigeria ni ya kina. Kulingana na taarifa za Telegraph Sport mwaka 2018, yeye ni miongoni mwa wajukuu wa Omo-Oba Daniel Adebambo Joshua, aristokrasia maarufu wa Sagamu anayejulikana kama Baba. Baba Josh alikuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa na mwanzilishi wa shule na kanisa mjini Sagamu, pamoja na kumiliki mali nyingi katika eneo hilo.
Familia ya Joshua ni miongoni mwa nyumba nne za kifalme zinazoweza kutoa mrithi wa cheo cha Akarigbo wa Remo, mfalme wa jadi wa eneo la Remo katika Jimbo la Ogun. Ingawa Joshua hazungumzi Kiyoruba kwa ufasaha, anaelewa na kuzungumza baadhi ya maneno ya lugha hiyo. Marafiki na jamaa humwita “Femi,” jina lake la kati linalomaanisha “Mungu Ananipenda.”
Mafunzo utotoni
Joshua aligusa kwa mara ya kwanza mila na tamaduni za Nigeria akiwa na umri wa miaka 11, alipokwenda kuishi huko baada ya mama yake kuanzisha biashara huko. Alisoma katika shule ya bweni ya The Bells mjini Ikenna, ambako alijifunza nidhamu kali iliyomjenga sana kimaisha.
Katika maelezo yake, Joshua amesema shule za Nigeria zilimfundisha mpangilio wa maisha, heshima kwa wakubwa, kujitegemea na kujilinda. Alijifunza lugha ya Kiyoruba, misemo yake, na namna ya kuishi katika mazingira magumu. Aliporudi Uingereza miezi sita baadaye, alihisi alikuwa mwenye nguvu zaidi kimwili na kiakili kuliko rika zake.
Ingawa nidhamu hiyo ilikuwa kali, Joshua anakiri kuwa ilimjenga na kumsaidia kukua kuwa mtu aliyeko leo.
Ndoto za Olimpiki
Kabla ya mafanikio yake na Timu ya Uingereza, Joshua aliwahi kutamani kuwakilisha Nigeria katika Olimpiki za Beijing 2008. Hata hivyo, kwa sababu ya kuchelewa kuhudhuria majaribio, hakupata nafasi hiyo. Hatimaye, alivaa jezi ya Uingereza na kushinda medali ya dhahabu katika Olimpiki za London 2012.
Licha ya hayo, uhusiano wake na Nigeria haukukatika. Joshua ana tattoo ya ramani ya Afrika mkononi mwake, huku Nigeria ikionyeshwa wazi, kama ishara ya utambulisho na uwakilishi wa watu wake.
Mchango nyumbani
Baada ya miaka 17 bila kurejea Nigeria, Joshua alirudi mwaka 2019 baada ya kupoteza mataji yake kwa Andy Ruiz Jr. Alichagua kurejea nyumbani kama mtu wa kawaida, si bingwa, ili kuungana tena na watu wake. Tangu wakati huo, uhusiano wake na Nigeria umeimarika zaidi.
Mwaka 2024, Joshua aliteuliwa kuwa balozi wa michezo wa Jimbo la Ogun, na serikali ya jimbo ilitangaza mpango wa kujenga ukumbi wa ndondi kwa heshima yake. Pia ameeleza nia ya kuanzisha akademi ya ndondi Nigeria baada ya kustaafu.
Kupitia taasisi yake, Joshua amesaidia jamii kwa kutoa misaada ya chakula, mahitaji muhimu wakati wa janga la Covid-19, na kusaidia zaidi ya watu 5,000 mjini Shagamu mwaka 2022.
Mama yake Yeta na dada yake Janet wamesisitiza kuwa familia yao ina dhamira ya dhati ya kurudisha kwa jamii, iwe ni Uingereza au Nigeria. Kwa Anthony Joshua, Nigeria si tu nchi ya asili ni nyumbani.