
Naibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha uvunii unaoneshwa na vyombo vya habari vya Magharibi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifanya mkutano maalumu na waandishi wa habari siku ya Alkhamisi na kuongeza kuwa, inavyoonekana ni kwamba baadhi ya duru za Magharibi zinapenda sana kupata kisingizio cha kusema uongo na kuchochea chuki katika kila jambo.
Mohsen Shamsizadeh amesema hayo kujibu madai yaliyochapishwa katika vyombo vya habari vya Marekani na ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuwa: Gazeti la New York Times limedai katika makala moja kwamba Bw. Araqchi (Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran) alizungumza na vyombo vya habari siku ya Alkhamisi na kuthibitisha habari hiyo. Cha kushangaza zaidi ni kwamba, televisheni ya Kizayuni ya “International” imeukuza kupindukia uvumi huo. Inavyoonekana ni kwamba, baadhi ya duru za Magharibi zinapenda mno kutafuta kisingizio cha kusema uongo na kuchochea chuki katika kila jambo, hata mambo madogo yasiyoingia akilini.
Shamsizadeh pia amesema: “Ni jambo la kawaida kwa waziri au msemaji kuwa na mikutano ya mara kwa mara na vyombo vya mawasiliano ya umma na waandishi wa habari kuhusu masuala ya sera za kigeni, lakini mkutano kama huo wenye maelezo ambayo chombo hiki cha habari cha Marekani (gazeti la New York Times) kilidai ulifanyika siku ya Alhhamisi iliyopita, kimsingi haukuwepo kabisa.”
Gazeti la New York Times lilijifanya kuwanukuu maafisa watatu wa Jamhuri ya Kiislamu na kuzidi kutia chumvi kwa kudai kuwa eti wakati maandamano yalipozidi nchini Iran, maafisa wakuu wa serikali ya Iran walikiri katika mikutano na mazungumzo ya faragha kwamba Jamhuri ya Kiislamu “imeingia katika kipindi cha hatari mno.”