
Viongozi wa nchi washirika wa Ukraine wamekutana mjini Paris kujadili mustakabali wa usalama wa taifa hilo. Rasimu ya tamko la pamoja imesema kuwa Marekani iko tayari kuongoza mfumo wa kufuatilia na kuthibitisha usitishaji mapigano nchini Ukraine endapo makubaliano ya amani yatafikiwa na Urusi. Imeongeza kuwa Washington pia itajitolea kuunga mkono kikosi cha kijeshi cha kimataifa kinachoongozwa na Ulaya kitakachowekwa Ukraine endapo Urusi itashambulia tena baada ya kusitishwa kwa mapigano.
Kikosi hicho kinatarajiwa kutoa ulinzi na uhakika wa usalama kwa Ukraine kupitia anga, bahari na nchi kavu, sambamba na kusaidia kujenga upya na kuimarisha majeshi ya Ukraine. Marekani itachangia uwezo wake wa ujasusi, vifaa na usafirishaji, pamoja na ahadi ya kuunga mkono kikosi hicho endapo Urusi itashambulia tena. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliandaa leo mkutano wa kile kinachoitwa Muungano wa washirika wa Ukraine, wakiwemo viongozi wa Ulaya, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na wajumbe wa Marekani. Mkutano huo unalenga kutoa ahadi za dhahiri za kuilinda Ukraine na kuhakikisha amani ya kudumu.