Bei za mafuta zimepanda kidogo huku masoko ya hisayakifikia viwango vipya vya juu siku ya Jumanne, wakati wawekezaji duniani wakiendelea kufuatilia matukio yanayohusiana na Venezuela—nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta—pamoja na mwelekeo wa uchumi wa dunia.
Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu operesheni ya kushangaza ya Marekani nchini Venezuela, ukionya kuwa hatua hiyo “imedhoofisha wazi kabisa kanuni ya msingi ya sheria ya kimataifa.”
“Mataifa hayapaswi kutishia au kutumia nguvu dhidi ya umoja wa eneo au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote,” alisema Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Bei za mafuta zimekuwa zikiyumba yumba tangu shambulio la kushitukiza lililofanywa na Marekani Jumamosi mjini Caracas, lililosababisha kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro na mke wake kukamatwa na kupelekwa New York.
Wamekana mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya na mengineyo walipofikishwa mahakamani siku ya Jumatatu. Jaji aliagiza waendelee kushikiliwa hadi tarehe ya kusikilizwa kwa kesi inayofuata, Machi 17.
Ingawa Venezuela ina takriban robo ya hifadhi ya mafuta duniani, wachambuzi wanaonya kuwa ongezeko la haraka la uzalishaji litakwamishwa na changamoto kadhaa, zikiwemo miundombinu chakavu, bei za chini, na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa.
Licha ya wasiwasi wa kisiasa duniani, baadhi ya masoko makuu ya hisa yameanza mwaka mpya kwa rekodi mpya za juu, baada ya kuvunja rekodi mara kadhaa mwaka 2025.
Soko la Seoul lilipanda zaidi kwa 1% siku ya Jumanne na kuvuka pointi 4,500 kwa mara ya kwanza, likiungwa mkono na ongezeko kubwa la thamani ya hisa za kampuni ya chip SK hynix.
Hali hiyo kama hiyo pia imeshuhudiwa katika soko la hisa la Wall Street, ambapo Dow Jones ilimaliza siku kwa rekodi mpya Jumatatu, kutokana na ongezeko la bei ya hisa za makampuni ya teknolojia ya Amazon na Meta.
Huko London, soko kuu la FTSE 100 lilifikia kiwango kipya cha juu Jumanne, kikivuka pointi 10,000, huku wawekezaji wakitarajia kupunguzwa zaidi kwa viwango vya riba nchini Uingereza kwa mwaka 2026.