Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaweza kuwa imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa njia ya kuhuzunisha, lakini shabiki wake mmoja ameacha hisia ya kudumu kwenye mashindano hayo.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

DRC ilitolewa hapo jana katika hatua ya 16 bora na Algeria baada ya kupoteza kwa bao 1-0, mbweha wa jangwani wakipata goli la ushindi katika dakika za nyongeza.

Hata hivyo kivutio kikubwa huko Rabat kilikuwa ni raia wa Congo, Michel Kuka Mboladinga, anayejulikana sana kama shabiki “sanamu” wa nchi hiyo.

Akiwa amevalia mavazi yenye rangi tofauti, Nkuka amejizolea umaarufu kwa kusimama kimya katika mechi zote, akinua mkono wake wa kulia, akiwa amefungua kiganja chake na macho kuelekeza angani, ikiwa ni ishara ya mfano wa sanamu ya mwanasiasa mashuhuri nchini Congo aliyeuawa na Wabelgiji, Patrice Lumumba.

Michel Nkuka Mboladinga shabiki sugu wa Leopard ya Congo
Michel Nkuka Mboladinga shabiki sugu wa Leopard ya Congo AP – Mosa’ab Elshamy

Aina hii ya ushabiki iliwavutia si tu raia wa Congo, lakini wenyeji Morocco na hata jumuiya ya kimataifa, ambapo maelfu ya watu walishirikisha maudhui yake duniani kote kwenye mitandao ya kijamii na kuwa kivutio kikubwa kwenye mashindano ya mwaka huu.

Hapo jana Nkuka aliambatana na mamia ya mashabiki wa Kongo ambao safari yao kwenda Morocco ilifadhiliwa na serikali ya Kinshasa, lakini licha ya kuujaza uwanja, timu yake iliaga mashindano.

Amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na namna alivyojitokeza kuishabikia Leopard.
Amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na namna alivyojitokeza kuishabikia Leopard. AP – Mosa’ab Elshamy

Mashabiki wa Kongo wanasema kitendo cha Nkuka ni heshima kwa Lumumba na ishara ya fahari ya taifa, ushabiki wake pia ukichukuliwa kama ishara ya amani na upendo hasa wakati huu taifa lao linaposhuhudia utovu wa usalama kwenye eneo la mashariki.

Shabiki huyu hapo jana kwa mara ya kwanza alionkena akitokwa machozi na kushusha mkono wake chini baada ya Algeria kupata goli la ushindi, kitendo kilichovuta hisia ya mashabiki wa soka wanaofuatilia michuano hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *