Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa huo, Kiseo Nzowa, kuchukua hatua dhidi ya watumishi waliochelewesha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Msingi Muungano wilayani Mwanga.
Babu alitoa agizo hilo jana wakati wa ziara ya kukagua miradi ya elimu wilayani humo, baada ya kubaini kuwa shule hiyo ilipokea shilingi milioni 50 Aprili 19 mwaka jana, lakini hadi sasa ujenzi upo katika hatua ya msingi.
Alisema haiwezekani Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha elimu, huku baadhi ya watumishi wakizikalia bila kutekeleza miradi iliyokusudiwa.
Babu alieleza kuwa shule hiyo ina madarasa mabovu, hali inayowaathiri wanafunzi, na kuwataka watumishi wa umma kuacha visingizio na kusimamia miradi kwa uwajibikaji.
Kwa Upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Kisewo Nzowa ameahidi kufanyia kazi maelekezo hayo huku akikiri kufanyika kwa uzembe kwa watendaji kutokana na mradi huo kuanza nje ya wakati.