Kitendo cha kutekwa Maduro pamoja na mkewe Cilia Flores kwa tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya kilijibiwa haraka na Umoja wa Afrika. Umoja huo ulielezea “wasiwasi mkubwa” na kutoa wito wa kuheshimu kikamilifu uhuru wa mipaka na kila taifa kuwa na uhuru wa kudhibiti mipaka yake. Umoja wa Afrika umezitaka pande zote zinazohusika kujizuia, kuwajibika, na kuheshimu sheria ya kimataifa ili kulinda amani na utulivu wa kikanda.
Macharia Munene, Profesa wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani mjini Nairobi, Kenya, anasema inashangaza kwamba hilo limefanywa na nchi inayodai kutetea sheria za kimataifa. Profesa Munene ameiambia DW kuwa Venezuela ni mfano wa kile kinachoweza kutokea, wakati nchi ndogo hazifuati maagizo ya Marekani au mataifa mengine makubwa yenye nguvu.
“Ndiyo, kuna suala la rasilimali. Afrika ina utajiri mkubwa wa madini muhimu na rasilimali nyingine ambazo baadhi ya nchi zinazitamani na huenda zikajaribu kuwanyima wapinzani wao. Vyovyote itakavyokuwa, mara nyingi nchi za Afrika huishia kuwa wahanga wanaoteseka.”
Profesa Munene anabainisha kuwa swali lililopo ni jinsi gani wanavyoweza kujinasua na kujilinda kutokana na vitendo hivyo.
Serikali chache Afrika zimetoa kauli kali dhidi ya kitendo cha Marekani Venezuela
Remi Dodd, mchambuzi wa masuala ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kampuni inayokusanya taarifa ili kutambua hatari ya RANE, anasema kuwa serikali chache sana za Afrika zimekuwa na msimamo mkali dhidi ya kitendo cha Marekani nchini Venezuela.
”Nigeria imekuwa kimya kwa kiasi fulani, bila kulaani hatua ya Marekani. Hali ni hiyo hiyo kwa Misri, Ethiopia, Kenya na hata serikali ambazo zina historia ya kutumia kauli za kupinga ubeberu, kama vile Namibia, nazo pia zimekuwa kimya kwa kiasi kikubwa.”
Dodd ameiambia DW kuwa huenda baadhi ya serikali barani Afrika zina nia ya kutoharibu uhusiano wao na Marekani. Afrika Kusini ambayo Trump ameishutumu kwa madai ya ubaguzi na hata mauaji ya kimbari ya Wa Afrika Kusini Wazungu, au Afrikaner, imeviita vitendo vya jeshi la Marekani kama ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Uvamizi unakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa
Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini, DIRCO imesema uvamizi kama huo unakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unakataza matumizi ya nguvu dhidi ya uhuru wa kisiasa wa kila taifa.
Munene anadai kuwa Marekani inaweza pia kuwa inaangalia maliasili za Afrika. Mfano mmoja ni makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyohitimishwa hivi karibuni kati ya Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambapo kampuni za Marekani zinapata madini muhimu kwa ajili ya magari ya umeme, na vifaa vya kielektroniki, kwa kubadilishana na msaada wa kiusalama wa Marekani.
Kulingana na Munene, kikubwa kuliko jambo lolote kwa sasa ni hofu ya utayari wa Trump kuanzisha mashambulizi ya haraka ya kijeshi. Wasiwasi uliopo ni kuwa Marekani inaweza kumshambulia mtu yeyote, wakati wowote bila mataifa dhaifu kuweza kujilinda. Swali ni nani anafuata?
Mwaka uliopita Marekani ilifanya mashambulizi ya anga nchini Nigeria na Somalia kama sehemu ya kupambana na ugaidi kwenye maeneo ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu. Hata hivyo, Dodd anaamini kwamba hatari ya kitu kama kile kilichomtokea Maduro, kutokea barani Afrika ni ndogo.