Katika dunia inayozidi kuwa na misukosuko ya kisiasa na kiusalama, Ujerumani inatafuta washirika wapya wa kuaminika, hasa wakati mshirika wake wa jadi, Marekani, ameanza kuchukua hatua zinazotia wasiwasi kama vitisho dhidi ya Greenland na ushuru mkubwa kwa bidhaa za Ulaya. Ndiyo maana viongozi wakuu wa Ujerumani wameanza kuelekeza macho yao India.
Baada ya ziara za viongozi waliopita, sasa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anatarajiwa kuzuru India kuanzia Januari 11 hadi 13, ambapo atakutana na Waziri Mkuu Narendra Modi katika jimbo la Gujarat na baadaye kuzuru Bangalore kukutana na wawakilishi wa kampuni za Ujerumani. Ziara hiyo inaambatana na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara, ikionyesha uzito wake wa kiuchumi.
Ujerumani inaiona India kama mshirika muhimu kwa sababu ya ukuaji wake mkubwa wa kiuchumi (zaidi ya asilimia sita), tofauti na Ujerumani inayokabiliwa na mdororo wa uchumi. Aidha, India ni chanzo muhimu cha wafanyakazi wenye ujuzi na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Ujerumani.
Kibiashara, uhusiano wa Ujerumani na India unaongezeka, ingawa bado uko nyuma sana ukilinganishwa na China. Hata hivyo, China na Urusi zimekuwa changamoto kwa Ujerumani kutokana na masuala ya usalama na kisiasa, hali inayoifanya India ionekane kama mbadala muhimu.
Matumaini ya mikataba ya biashara ya silaha
Merz anaamini kuwa Ulaya inapaswa kujenga mfumo mpya wa biashara unaozingatia sheria, na kwamba ni muhimu kueneza minyororo ya biashara na malighafi kwa kushirikiana na nchi kama India.
Hata hivyo, uhusiano wa Ujerumani na India una changamoto, hasa kuhusu Urusi. India imeendelea kudumisha uhusiano mzuri na Urusi, ikinunua mafuta na silaha, licha ya vikwazo vya Magharibi. Wachambuzi wanaamini India haitabadilisha msimamo wake wa kujitegemea kimkakati.
Katika sekta ya ulinzi, India bado inategemea sana silaha za Urusi, ingawa nchi kama Ufaransa zimefanikiwa kupata mikataba mikubwa ya kijeshi na India. Ujerumani inatarajia kunufaika na mipango ya India ya kuliboresha jeshi lake, hasa kupitia mauzo ya ndege za kijeshi na manowari, na ziara ya Merz inaweza kuwa fursa muhimu kufanikisha hilo.