Ayatolla Khamenei anayeiongoza Iran tangu mwaka 1989 amesema waandamanaji wanaharibu nchi yao wenyewe ili kuifurahisha Marekani. Kiongozi huyo aliye na miaka 86 amesema nchi hiyo haitarudi nyuma kama maadui wa taifa hilo wanavyotaka. Ameonya kuwa Trump aliyemuita mtu mwenye kiburi atapinduliwa madarakani.
Hata hivyo Marekani kupitia makamu wake wa Rais JD Vance imeendelea kusema kwamba nchi hiyo inasimama pamoja na waandamanaji wa Iran.
“Tuko pamoja na yeyote anaejishughulisha na maandamano ya amani, yeyote anayejaribu kusimamia haki yake, ya sauti yake kusikika. Kwa hakika utawala wa Iran una matatizo mengi. Kama rais Trump alivyosema kitu kizuri kwao ni kufanya majadiliano ya kweli na Marekani kuhusu kile tunachotaka kukiona likija katika suala la mpango wao wa nyuklia. Ntamuacha rais Trump baadae azungumzie kile tunachotaka kukiona katika siku za usoni lakini kwa sasa tunasimama na watu wa iran wanaopigania haki.”
Iran imeendelea kukumbwa na maandamano makubwa yalioingia siku yake ya 13, yaliyochochewa na hasira kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha. Waandamanaji walimiminika barabarani wakisema kwa sauti “Kifo kwa dikteta” wakimlenga moja kwa moja Ayatollah Ali Khamenei, huku wakichoma moto majengo ya serikali.
Serikali imekata huduma za intaneti kuanzia jana alhamisi na hadi sasa taifa hilo halijakuwa na huduma hiyo kwa saa 12. Kulingana na shirika linalofuatilia masuala ya mtandao Netblocks serikali imefanya hivyo kwa maksudi kudhibiti maandamano kuenea zaidi.
Reza Pahlavi, mwana wa kiongozi wa utawala wa zamani wa mfalme Mohammad Reza Pahlavi nchini Iran, aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi ya kiislamu ya mwaka 1979, ndiye anayetoa wito wa maandamano makubwa zaidi kufanyika nchini humo. Reza Pahlavi anayeungwa mkono na Marekani, amesema idadi kubwa ya watu barabarani inaudhoofisha utawala uliopo na kuulazimisha kuachia ngazi.
Shirika la habari la AFF limeonyesha video ya waandamanaji wakipiga honi, huku moshi ukionekana ukifuka katika vituo vya televisheni vya taifa. Maandamano yameshuhudiwa Tabriz, iliyoko kaskazini mwa Iran pamoja na mji mtakatifu wa Mashhad, upande wa masharik. Maeneo yaliyojaa wakurdi upande wa Magharibi pia maandamano yameshuhudiwa huko.
Maandamano ya leo Ijumaa (09.01.2026), yanasemekana kuwa makubwa tangu mwaka 2022 wakati wa maandamano ya kupinga kifo cha msichana wa miaka 22 Mahsa Amini kilichotokea akiwa kizuizini, baada ya kukamatwa kwa kosa la kutovalia hijabu.
Makundi ya kutetea haki za binaadamu yameishutumu Iran kuwaua waandamanaji kwa kuwafyatulia risasi lakini vidio za hivi karibuni kutoka Tehran hazijaonyesha maafisa wa usalama wakiwaandamana waandamanaji hao.
Huku hayo yakiarifiwa Ufaransa imesema Iran ni lazima iwe na uvumilimu dhidi ya waandamanaji walio na haki ya kuandamana huku ikiitaka Jamhuri hiyo ya kiislamu kuanzisha uchunguzi mara moja, kuhusu mauaji ya waandamanaji yaliyoripotiwa. Ufaransa imesema inatambua uhuru wa kujieleza na kuitaka Iran iheshimu hilo, chini ya wajibu wake wa kimataifa.
