Maandamano nchini Iran yalizuka Disemba 28 na kusambaa kote nchini humo, wakati waandamanaji wakionyesha kutoridhika kwao na hali ya uchumi inayozidi kuwa mbaya pamoja na kuanguka kwa sarafu yake. Watu kadhaa wameuawa na maelfu wamekamatwa huku maandamano ya kila siku yakiongezeka na serikali ikiangalia namna ya kuyadhibiti.
Ingawa lengo la awali lilijikita kwenye masuala kama vile kupanda kwa bei za vyakula muhimu na kiwango cha mfumuko wa bei cha kila mwaka nchini, waandamanaji sasa wameanza kutoa kauli za kuipinga serikali pia.
Maandamano yalianzaje?
Disemba 28: Maandamano yalianza kwenye masoko makubwa katikati ya mji mkuu Tehran, kufuatia anguko kubwa kabisa la sarafu ya Iran ya riya la hadi milioni 1.42 dhidi ya dola ya Marekani, hatua iliyochochea mfumuko mkubwa wa bei wa vyakula na mahitaji mengine ya kila siku. Na hatua ya serikali ya kupandisha bei za petroli inayotolewa ruzuku kitaifa mapema Disemba, ilichochea hata zaidi ghadhabu ya umma.
Disemba 29: Mkuu wa Benki Kuu Mohammad Reza Farzin alijiuzulu huku maandamano yaliyoanzia mjini Tehran yakienea hadi miji mingine. Polisi wakaanza kuwafyatulia gesi ya kutoa machozi waandamanaji ili kuwatawanya katika mji huo mkuu.
Disemba 30: Huku maandamano yakienea kwenye miji mingi zaidi pamoja na vyuo vikuu kadhaa, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alikutana na kundi la viongozi wa biashara ili kusikiliza madai yao na kuahidi kwamba utawala wake “hautaacha kufanya juhudi za kila hali ili kutatua matatizo yaliyopo” pamoja na uchumi.
Iran yamteua gavana mpya wa Benki Kuu
Disemba 31: Iran inamteua Abdolnasser Hemmati kama gavana mpya wa Benki Kuu. Maafisa kutoka upande wa kusini mwa Iran wanasema kwamba maandamanao kwenye mji wa Fasa yamebadilika na kuwa ghasia baada ya makundi ya waandamanaji kuvamia ofisi ya gavana na kuwajeruhi maafisa wa polisi.
Januari 1: Kwa mara ya kwanza kunaripotiwa vifo na majeruhi ya waandamanaji. Mamlaka zinasema karibu watu saba wameuawa Machafuko makubwa kabisa yanashuhudiwa pia kwenye jiji la Azna, ulioko kwenye jimbo la Lorestan ambako video zilizochapishwa mitandaoni zilionyesha vitu vikiwaka moto barabarani na milio ya risasi ikisikika huku watu waandamanaji wakisema kwa kelele: “Aibu! Aibu! Shirika la habari lenye mafungamano kwa kiasi na serikali, Fars liliripoti viof vya watu watatu. Waandamanaji wengine waliripotiwa kuuawa kwenye majimbo ya Bakhtiari na Isfahan, huku kijana wa umri wa miaka 21 aliyekuwa akijitolea kwenye Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Basij akiuawa katika eneo la Lorestan.
Januari 2: Rais Donald Trump wa Marekani anaibua sintofahamu zaidi, baada ya kuandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba ikiwa Iran “itawaua kikatili watu wanaoandamana kwa amani” Marekani “itakuja kuwaokoa.” Onyo hilo, linalotolewa miezi kadhaa baada ya vikosi vya Marekani kushambulia maeneo ya nyuklia ya Iran, linajumuisha matamshi ambayo hayakufafanuliwa: “Tumejiandaa na tuko tayari kwenda.” Wakati huo huo, maandamano yanaongezeka na kufikia zaidi ya maeneo 100 katika majimbo 22 kati ya 31 ya Iran, kulingana na Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu lenye makao yake Marekani, HRANA.
Khamenei: “waandamanaji wawekwe mahali panapostahili”
Januari 3: Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei anasema “waandamanaji lazima wawekwe mahali panapostahili,” katika kile kinachoonekana kama kuviruhusu vikosi vya usalama kuanza kudhibiti maandamano kwa hatua kali zaidi. Maandamano yanaongezeka hadi kwenye zaidi ya maeneo 170 katika majimbo 25, huku angalau watu 15 wakiuawa na 580 wakikamatwa, HRANA inaripoti.
Januari 6: Waandamanaji wanakusanyika mbele ya jengo la manunuzi la Grand Bazaar mjini Tehran hadi vikosi vya usalama vinapowatawanya kwa kutumia gesi ya machozi. Idadi ya vifo inaongezeka hadi 36, wakiwemo wanajeshi wawili wa vikosi vya usalama vya Iran, kulingana na HRANA. Maandamano yamefikia zaidi ya maeneo 280 katika majimbo 27 kati ya 31 ya Iran.
Januari 8 – 9: Kufuatia wito kutoka kwa mwanamfalme wa Iran aliye uhamishoni, Reza Pahlavi, ambaye baba yake alikimbia Iran muda mfupi kabla ya kuzuka kwa Vuguvugu la Kiislamu mnamo mwaka 1979, umati wa watu uliandamana mitaani usiku kucha. Serikali inajibu hilo kwa kuzuia intaneti na simu za kimataifa, katika juhudi za kuizuia nchi hiyo yenye watu milioni 85 dhidi ya ushawishi wa nje. HRANA inasema vurugu zinazojitokeza kwenye maandamano hayo zimesababisha vifo vya watu wasiopungua 42 huku wengine zaidi ya 2,270 wakikamatwa.