Khamenei amesema kuna watu wanaofanya kila juhudi kusababisha uharibifu ili kumfurahisha rais wa Marekani Donald Trump. Amesisitiza kwamba taifa lake halitamkinga mtu yeyote aliye na nia ya kuvuruga amani na utulivu huku akisema taifa hilo halitovumilia visa vya huduma za kimamluki kwa mataifa ya nje.
“Jana usiku mjini Tehran na katika miji mengine watu walijitokeza na kuharibu majengo yao wenyewe na kuharibu maeneo yao ili kumfurahisha rais wa taifa jengine.”
Kiongozi huyo wa Iran alioko madarakani tangu mwaka 1989 amesema nchi hiyo haitarudi nyuma kama maadui wa taifa hilo wanavyotaka. Ameonya kuwa Trump aliyemuita mtu mwenye kiburi atapinduliwa madarakani huku akisema mikono ya rais huyo wa Marekani, imejaa damu ya wairani wakati wa vita vya siku 12 kati ya taifa hilo na Israel.
Ayatolla Ali Khamenei amesema Trump aliyema atakuja kuwaokoa waandamanaji anapaswa kushughulikia kwanza matatizo yaliyopo nchini mwake.
“Mikono yake imejaa damu ya maelfu ya wairani waliouwawa katika siku 12 za mapigano kati yetu na Israel mwaka 2025. Kisha anasema anauwaunga mkono watu wa Iran, na watu ambao hata hawafikirii hata kidogo wanamsikiliza na kumuamini, wakichoma moto maeneo yao ili kumfurahisha.”
Hadi sasa Marekani haijasema chochote kuhusu kauli za Khamenei.
Gholamhossein: Adhabu dhidi ya waandamanaji itakuwa kali
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa taifa hilo Gholamhossein Mohseni-Ejei amesema adhabu kwa waandamanaji itakuwa nzito na ya haraka isiyokuwa na huruma. Trump mara kwa mara amekuwa akitoa vitisho vya kutumia nguvu za kijeshi Iran iwapo Jamhuri huiyo ya kiislamu haitaacha kile alichosema ni mauaji dhidi ya waandamanaji.
Wakati huo huoripoti za mauaji zinaendelea kusikika, baada ya vikosi vya usalama kudaiwa kuwamiminia risasi waandamanaji jana Alhamisi. Video ambazo bado hazijathibitishwa zilizosambaa mitandaoni zinawaonesha vijana ambao nguo zao zimelowa damu wakiwa sakafuni nje kidogo ya mji wa Tehran. Hadi sasa inasemekana watu 42 wameuwawa ndani ya siku 13 za maandamano Iran huku zaidi ya 2000 wakimakatwa.
Safari za ndege kuelekea Iran zafutwa
Hali inayoendelea nchini Iran imesababisha mashirika kadhaa ya ndege kufuta safari zao huko, likiwemo shirika la ndege la Uturuki, lililofuta safari zake kuelekea miji ya Tehran, Mashhad na Tabriz. Shirika la ndege za bei nafuu la Pegasus pia limefuta safari zake Iran.
Jamhuri hiyo ya kiislamu imeendelea kushuhudia maandamano makubwa ya kupinga, kupanda kwa gharama ya maisha, kudorora kwa uchumi na sera mbovu za serikali zinazodaiwa kuididimiza nchi hiyo katika hali mbaya ya kiuchumi. Katika kile kinachosemekana kuwa ni kujaribu kuyadhibiti maandamano serikali imekata huduma ya intaneti kuanzia jana Alhamisi.
Umoja wa Ulaya umekasirishwa na hatua hiy na kutoa wito kwa utawala nchini humo kurejesha huduma hiyo mara moja na kukosoa vurugu za aina yoyote dhidi ya waandamanaji. Msemaji wa Umoja huo Anouar El Anouni amesema watu wa Iran wanatetea haki yao ya kuwa na maisha bora.