
Zaidi ya raia wa Kongo 50 waliokimbia vita mashariki mwa nchi yao wamekufa nchini Burundi, hayo yamesemwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilipozungumza na shirika la habari la Reuters.
Shirika hilo limesema kati ya jumla ya vifo 53 vilivyorekodiwa, watu 25 wamekufa kutokana na mlipuko wa kipindupindu, huku wengine sita wakifariki kutokana na upungufu wa damu na matatizo mengine yanayohusiana na utapiamlo.
UNHCR imeongeza kwamba zaidi ya Wakongo laki moja wametafuta hifadhi nchini Burundi tangu mapigano yalipozidi mapema Desemba na waasi kuuteka mji wa Uvira.
Jean Jacques Purusi, gavana wa jimbo la Kivu Kusini ambapo Uvira iko, ameieleza hali inayowakabili raia wa Kongo waliokimbilia Burundi kuwa ni ya “taabu” na kwamba ni mgogoro uliosahaulika na jamii ya kimataifa. Burundi kwa upande wake haijatoa maoni juu ya taarifa hiyo.