Yi ametoa matamshi hayo alipokuwa akihitimisha ziara yake kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa China hakutaja mahala popote machafuko ya kisiasa yaliyoigubika Tanzania mwezi Oktoba na Novemba mwaka jana ambayo yameyumbisha mahusiano ya serikali mjini Dodoma na washirika wake wa nchi za Magharibi.
Wang Yi ni waziri wa kwanza wa mambo ya kigeni kuitembeleaTanzania tangu palipotokea ukandamizaji mkubwa wa waandamanaji waliokuwa wakipinga uchaguzi wa mwaka jana.
Taarifa yasema China imesifu uchaguzi mkuu wa 2025
Upinzani nchini Tanzania unasema watu wasiopungua 2,000 waliuawa na vikosi vya usalama wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa rais na bunge ambao waangalizi wa kimataifa wamesema ulikuwa na dosari na vitendo vyavyoashiria udanganyifu.
China, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imewekeza sana nchini Tanzania, haikutoa tamko lolote kuhusu ukandamizaji huo uliozusha ukosoaji mkubwa wa kimataifa na hata kupelekea Marekani kutangaza kupitia upya mahusiano yake na nchi hiyo.
Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya ziara ya Yi, mamlaka nchini Tanzania zimesema waziri huo aliipongeza nchi hiyo kwa “kuandaa kwa mafanikio” makubwa uchaguzi wa mwaka jana.
“China imesisitiza juu ya imani yake kwa uongozi wa Tanzania na taasisi zake katika kuendesha na kusimamia masuala yake ya ndani kwa uhuru,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Wakati huohuo, taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China imesema serikali mjini Beijing “inapinga shinikizo lolote kutoka nje kwa masuala ya ndani ya Tanzania” na kusisitiza kwamba inaunga mkono “uhuru na usalama wa taifa” hilo.
Tanzania yasifu mahusiano ikiwemo ya kibiashara na China
Wakati wa ziara hiyo waziri Wang alikutana pia na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alishinda kiti cha urais kwa asilimia 98 ya kura.
Alisisitiza “uungaji mkono wa China kwa Tanzania”, wakati wa mkutano wao. Hayo yamesemwa kwenye taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Tanzania.
Taarifa hiyo imesema kumetolewa pia ahadi ya kuimarishwa uhusiano baina ya pande hizo mbili na kutambua kutanuka kwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.
Tanzania imesema mafanikio hayo yametokana na sera ya China ya kufungua masoko yake kwa bidhaa kutoka Afrika.
China imeimarisha uwekezaji wake nchini Tanzania hasa kwenye kongoni za viwanda zinazotoza kiwango kidogo cha kodi, ambako miradi ipatayo 343 yenye thamani ya dola bilioni 1.3 ilisajiliwa mwaka jana pekee. Takwimu hizo ikiwa ni kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Tanzania.