Kadri Uganda inavyokaribia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 15 Januari 2026, kuna mtu mmoja anayetikisa mijadala ya kisiasa kuliko wengine wote: Bobi Wine. Kwa wafuasi wake, yeye ni mfano wa matumaini na mabadiliko ya kizazi. Kwa dola, yeye ni changamoto endelevu kwa mfumo uliotawala bila kukatizwa kwa karibu miongo minne.
Amezaliwa kama Robert Kyagulanyi Ssentamu katika mitaa duni ya Kampala, kupanda kwa Bobi Wine hakukuwa kwa njia ya kawaida. Alikulia katika mazingira ya umaskini, manyanyaso ya polisi na ukosefu wa fursa — hali ambazo baadaye ziliunda muziki na siasa zake. Kabla hata ya kuingia bungeni, Wine alikuwa tayari jina maarufu kupitia nyimbo za dancehall na reggae zilizozungumzia moja kwa moja maisha ya maghetto ya mijini nchini Uganda.
Nyimbo zake zilibadilika taratibu kutoka kuwa za burudani na sherehe hadi muziki wa maandamano, zikikosoa waziwazi ufisadi, ukosefu wa usawa na ukandamizaji wa dola. Katika nchi ambako wasanii mara nyingi wanatarajiwa kuunga mkono walio madarakani, uasi wa Wine ulimtofautisha na kumpatia uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa vijana na wafanyakazi wa kawaida.
Uganda imetawaliwa tangu mwaka 1986 na Rais Yoweri Museveni, ambaye amebadilisha katiba kuondoa ukomo wa umri na mihula ya urais. Kwa Waganda wengi walio chini ya umri wa miaka 35 — ambao ni sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini humo — Museveni ndiye rais pekee waliyewahi kumjua.
Kutoka muziki hadi bungeni
Bobi Wine aliingia rasmi katika siasa mwaka 2017 aliposhinda kiti cha ubunge, akiwashinda wagombea walioungwa mkono na chama tawala cha National Resistance Movement, NRM. Ushindi huo uliashiria mabadiliko katika taswira ya kisiasa ya Uganda na kuthibitisha uwezo wake wa kubadilisha umaarufu wa muziki kuwa nguvu ya kisiasa.
Mabadiliko hayo yalionekana wazi katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021. Akigombea dhidi ya Museveni, Wine alipata asilimia 35 ya kura, huku rais huyo aliyeko madarakani akipata asilimia 58 — matokeo mabaya zaidi kwa Museveni katika miongo kadhaa. Wine alidai kulikuwa na udanganyifu mkubwa, kupachikwa kwa kura na vitisho kwa wapiga kura, madai ambayo tume ya uchaguzi ilikanusha.
Tangu wakati huo, Wine anasema ukandamizaji dhidi ya harakati zake umeongezeka. Chama chake, National Unity Platform, NUP, kinasema wafuasi wake kadhaa wamefungwa, kutekwa nyara au kupotea. Mikusanyiko ya kisiasa mara nyingi huzuiwa, na kampeni hukumbana na gesi ya machozi, kukamatwa na vipigo.
Licha ya mashaka ya awali kuhusu iwapo angeruhusiwa kugombea mwaka 2026, Wine aliteuliwa rasmi kuwa mgombea urais wa NUP mwezi Septemba 2025. Tangazo hilo lilifufua hamasa miongoni mwa wafuasi wake — na pia kuongeza mvutano na vyombo vya usalama.
Mwezi Desemba 2025, Wine na wanachama wa timu yake ya kampeni walishambuliwa na kupigwa na vikosi vya usalama walipokuwa wakifanya kampeni katika mji wa Gulu kaskazini mwa Uganda. Picha na video za tukio hilo zilisambaa haraka mtandaoni, zikiongeza hofu kuhusu kupungua kwa nafasi ya siasa za upinzani.
Kampeni chini ya vitisho
Wine anasema hatari ni ya kudumu, lakini ndivyo ilivyo pia hamasa. “Kila siku kuna sababu 99 zinazotufanya tuachane na mapambano kwa sababu ni hatari,” alisema. “Lakini kuna sababu moja kubwa ya kuwa jasiri — upendo, hamasa, uungwaji mkono na mshikamano.”
Hofu kuhusu usalama wake imechochewa na vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa mwana wa rais na mkuu wa majeshi, Muhoozi Kainerugaba. Katika chapisho moja la mitandao ya kijamii, Kainerugaba alipendekeza kuwa angeweza “kukata kichwa” cha Wine kama angeruhusiwa — kauli iliyozua ukosoaji mkali kimataifa.
Mmoja wa walinzi wa Wine baadaye alionekana mahakamani akiwa hawezi kutembea bila msaada, ishara ya wazi ya mateso baada ya kuripotiwa kupotea. Kwa Wine, ujumbe ni wazi.
“Huyu si mtu wa kawaida,” alisema. “Anaongoza jeshi, polisi, magereza… yuko juu ya sheria.”
Hata hivyo, ukandamizaji haujapunguza dhamira ya harakati hizo. Wine mara nyingi hujitaja kama “rais wa gheto,” akisisitiza mizizi yake na uhusiano wake na Waganda wa kawaida wanaopambana na ukosefu wa ajira na gharama ya juu ya maisha.
Vijana, upinzani na safari iliyo mbele
Msingi wa uungwaji mkono wa Wine ni vijana kwa wingi. Wengi wanaona uchaguzi wa 2026 kama hesabu ya kizazi — fursa ya hatimaye kuwakilishwa.
“Tunaenda kumchagua kiongozi wetu, Bobi Wine,” alisema mfuasi wake Joel Katumba. “Museveni atapanga matokeo, lakini tutatembea kwa njia ya amani.”
Kwa wengine, tatizo ni kukosekana kabisa kwa uwakilishi wa kizazi.
“Ameiwakilisha kizazi chake,” alisema Ruth Excellent Mirembe. “Lakini sisi kama Gen Z na milenia tunakosa uwakilishi.”
Safari ya Wine haijakosa utata. Nyimbo zake za zamani zilizokosolewa kwa chuki dhidi ya mashoga, migogoro ya hadharani na wanamuziki wanaoiunga mkono serikali, pamoja na kukamatwa mara kwa mara, vimeibua maswali. Kwa muda, amejijenga upya kama mtetezi wa uanaharakati wa amani na uvumilivu.
Kimataifa, Wine amekuwa ishara ya upinzani wa kidemokrasia. Filamu ya waraka ya mwaka 2022 iliyoeleza mapambano yake ilipata uteuzi wa Tuzo ya Academy, na kuleta uangalizi wa dunia kwa mgogoro wa kisiasa wa Uganda.
Kadri Uganda inavyokaribia Januari 2026, Bobi Wine yuko katikati ya makutano ya kihistoria — mwanamuziki aliyebadilika kuwa mwanasiasa, akiweka maisha yake hatarini kumkabili mmoja wa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika. Awe mshindi au la, harakati zake tayari zimebadilisha siasa za Uganda na kuamsha kizazi kilichoamua kutonyamazishwa.
