Serikali ya Uganda imetangaza likizo ya siku mbili kwa wananchi kushiriki uchaguzi mkuu siku ya alhamisi wikik hii, ambapo rais Yoweri Museveni atashindana na kinara wa upinzani, Robert Kyagulanyi.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Katika jiji kuu la Kampala, baadhi ya wakaazi wameanza kusafiri kwenda vijijini au Charo kwa lugha ambayo wanaielewa kushiriki kura za Alhamisi.Wanaopiga kura mjini wapo kwenye kipindi cha lala salama ya kuhamasishana.

Nimetembea sehemu mbali mbali kuelewa kikubwa kinachowashawishi kupiga kura. Wafuasi wa chama tawala cha NRM walikuwa na haya.

“Tunakaa vizuri, hakuna kelele, tunamtaka mzee Museveni aende mbele hadi achoke. ”

“Mimi nataka kumpigia Rais Museveni kura sio mtu mwengine, anatuongoza vizuri sana. ”

Na wanaounga mkono upinzani wengi wao wakiwa vijana, jambo lao kubwa ni hili?

“Tumechoka, tunataka kuibadilisha Uganda, Tunataka Uganda mpya. ”

“Tunaenda kumfukuza Rais Museveni, saa hii hakuna dawa hospitalini.”

Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika Jumuiya ya Madola, IGAD na hata ukanda wa maziwa makuu wamewasili kufuatilia uchaguzi huo muhimu.

Deo Mwapinga ni katibu mkuu wa waangalizi wa maziwa makuu.

“Misingi ya demokrasia katika uchaguzi inaelezwa na sheria za ndani za nchi, iwe ni katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na tunatarajia wadau wote wa ndani wataheshimu. ” Alisema Deo Mwapinga katibu mkuu wa waangalizi wa maziwa makuu.

Tume ya uchaguzi imeorodhesha wapiga kura zaidi ya milioni 21 wanaotarajiwa kushiriki zoezi hili.

Carol Korir, Kampala RFI Kiswahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *