
Kampuni ya Meta imefunga zaidi ya akaunti 544,000 za mitandao ya kijamii zinazomilikiwa na watoto, kufuatia sheria mpya ya Australia ya mitandao ya kijamii.
Sheria hiyo, iliyoanza kutumika Desemba 10, inapiga marufuku watoto walio chini ya umri wa miaka 16 kumiliki akaunti za mitandao ya kijamii na inayataka majukwaa makubwa kama Meta, TikTok na YouTube kuondoa akaunti hizo.
Kampuni ambazo zitakosa kuchukua hatua stahiki kulingana na sheria hiyo, zitakabiliwa na faini had idola za Australia milioni 49.5.
Mmiliki wa Meta, bilionea Mark Zuckerberg ameainisha kwamba miongoni mwa akaunti walizofunga kati ya Desemba 4 na Disemba 11 ni 330,639 za Instagram, 173,497 za Facebook na 39,916 za Threads.
Meta imesema inazingatia sheria hiyo, lakini bado ina wasiwasi kuhusu namna ya kubaini umri mtandaoni.
Kampuni hiyo imetoa wito kwa serikali ya Australia kushirikiana na sekta ili kupata njia bora, badala ya marufuku ya jumla.