Maelfu ya raia wa Iran wamemiminika mitaani siku ya Jumatatu kama ishara ya kuiunga mkono serikali chini ya Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na kuomboleza vifo vya maafisa wa usalama waliouawa wakati wa maandamano hayo.
Watu waliokuwa wamebeba bendera ya jamhuri ya Kiislamu ya Iran walifurika katika Uwanja wa Mapinduzi mjini Tehran. Mikusanyiko kama hiyo imeripotiwa pia katika miji mingine baada ya wito wa Rais Masoud Pezeshkian wa kuwataka watu kupinga kile kinachotajwa na utawala kuwa ni “machafuko”.
Akihutubia umati mjini Tehran, Spika wa Bunge la Iran amezituhumu Marekani na Israel kwa kuchochea maandamano hayo huku akilitaja jibu la kukabiliana na wimbi la maandamano yaliyoitikisa jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa wiki mbili kuwa ni “vita dhidi ya magaidi”. Mohammad Bagher Ghalibaf amesema Iran inapigana “vita vya pande nne na Marekani na Israel ambavyo ni vita vya kiuchumi, kisaikolojia, kijeshi na leo hii vita dhidi ya magaidi na kwamba taifa kubwa la Iran halijawahi kumruhusu adui kufikia malengo yake.
“Jeshi la Iran litamfundisha Rais wa Marekani Donald Trump “somo lisilosahaulika” iwapo kutakuwa na shambulio jipya, alisisitiza Spika huyo wa Bunge la Iran.
Msimamo wa Iran, Marekani na EU
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumatatu kuwa Iran iko tayari kwa mazungumzo baada ya kutishia kuishambulia kutokana na vitendo vya ukandamizaji na mauaji dhidi ya waandamanaji.
Kauli ya Trump ilitolewa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Oman ambayo kwa muda mrefu imekuwa mpatanishi kati ya Washington na Tehran kufanya ziara huko Iran mwishoni mwa juma iliyopita.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amerejelea kauli yake kuwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu iko tayari kwa mazungumzo na Marekani lakini akasisitiza pia kuwa Iran imejiandaa “kikamilifu” kwa vita.
Mataifa mbalimbali yamekosoa hatua ya serikali mjini Tehran . Umoja wa Ulaya kupitia msemaji wake Anouar El Anouni umesema “unatathmini” uwezekano wa kuiwekea vikwazo vipya na vikali zaidi Iran kutokana na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji.
Hayo yakiarifiwa, kundi la kutetea haki za binaadamu lenye makao yake nchini Marekani, la HRANA, limesema limethibitisha vifo vya waandamanaji 490 na maafisa 48 wa usalama, huku zaidi ya watu 10,600 wakikamatwa tangu kuanza kwa maandamano hayo mnamo Desemba 28 mwaka jana na ambayo yameenea kote nchini humo.
Hata hivyo idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa na vyombo huru vya habari kutokana na kuzimwa kwa mtandao wa Intaneti tangu Alhamisi wiki iliyopita.