
Akizungumza mjini Nairobi baada ya kutembelea kambi ya wakibizi ya Kakuma kaskazini mwa Kenya, Salih ameipongeza Kenya kwa dhamira yake ya muda mrefu ya kuwahifadhi wakimbizi na sera zake za maendeleo zinazowezesha wakimbizi kufanya kazi, kupata elimu na huduma za afya, pamoja na kushiriki kikamilifu katika uchumi.
“Licha ya rasilimali chache, Kenya inaendelea kuonesha mshikamano wa kipekee kwa watu wenye mahitaji kupitia sera madhubuti zinazokuza kujitegemea na ukuaji wa uchumi,” amesema Salih.
Ameongeza kuwa “Kakuma ni eneo la mabadiliko na ubunifu, likitoa ujumbe wenye nguvu kwa dunia, badala ya kuwafungia wakimbizi katika utegemezi wa misaada, ni lazima tutilie mkazo kwa dharura suluhu zinazowawezesha kuishi kwa heshima na kuchangia katika jamii.”
Mfumo wa Kenya unaendelea kukabiliwa na shinikizo
Kwa mujibu wa UNHCR Kenya inawahifadhi zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi 800,000, wakiwemo takriban 300,000 wanaoishi Kakuma, wengi wao wakitoka Sudan Kusini, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Ingawa nchi hiyo imetambuliwa kwa sera zake jumuishi kwa wakimbizi, Salih aameonya kuwa mafanikio hayo yako hatarini kutokana na uhaba mkubwa wa ufadhili.
Mwaka jana, chini ya robo ya bajeti ya UNHCR ya mahitaji kwa Kenya ndiyo ilipatikana, hali iliyosababisha kupunguzwa kwa huduma muhimu kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.
Huduma za afya, maji na elimu zimepunguzwa, huku mifumo ya ulinzi ikikabiliwa na shinikizo kubwa.
Salih amesema “Vituo vya mapokezi vimefurika, na huduma muhimu kwa watoto na waathirika wa ukatili wa kijinsia zinaendelea kupunguzwa. Mgogoro wa ufadhili unatishia maisha na una hatari ya kufuta mafanikio yaliyopatikana kwa juhudi kubwa.”
Njia ya kuelekea kujitegemea
Kiini cha ujumbe wa Salih ni Mpango au mfumo wa UNHCR unaoongozwa na Serikali ya Kenya unaolenga kuondoka katika misaada ya kibinadamu ya muda mrefu na kuelekea kujitegemea kwa wakimbizi pamoja na kuishi kwa amani na jamii zinazowahifadhi.
Chini ya Mpango huu, wakimbizi wanaweza kupata nyaraka halali za utambulisho, vibali vya kazi, huduma za fedha za kidijitali na benki, elimu ya umma na huduma za afya kwa wote.
“Sera hizi jumuishi zina ahadi kubwa ya kubadilisha mustakabali wa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi,” amesema Salih akiongeza kuwa “Hata hivyo, mafanikio yake yatategemea hatua za haraka kutoka kwa wadau wa maendeleo, taasisi za fedha za kimataifa, wafadhili na sekta binafsi.”
Mikutano ya ngazi ya juu Nairobi
Wakati wa ziara yake, Kamishna Mkuu amekutana na Rais William Ruto pamoja na maafisa wengine wakuu wa serikali, akipongeza uongozi wa Kenya na dhamira yake ya kisiasa katika kuendeleza sera za wakimbizi zilizo jumuishi.
Amesema “Jukumu la kihistoria la Kenya katika kuwakaribisha wakimbizi ni mfano muhimu wakati ambapo mshikamano wa kimataifa uko katika shinikizo.”
Amemshukuru Rais Ruto kwa kuendeleza sera zinazotanguliza heshima, ujumuishaji na ustawi wa pamoja.
Kadri migogoro na ufurushwaji wa watu unavyoendelea kuongezeka duniani, Salih amesisitiza kuwa uzoefu wa Kenya unaonesha wazi kuwa kwa sera sahihi na uungwaji mkono wa kutosha, wakimbizi wanaweza kuwa wachangiaji wa maendeleo badala ya kuonekana kama mzigo.