Usiku wangu katika kijiji cha wanawake nchini KenyaUsiku wangu katika kijiji cha wanawake nchini Kenya

Katika Kaunti ya Samburu, kaskazini mwa Kenya, kuna kijiji kinachoongozwa na sheria moja kuu: wanaume hawaruhusiwi kuishi wala kulala hapa.

Kwa zaidi ya miongo mitatu, kijiji cha Ltungai kimekuwa mfano wa kijiji cha wanawake pekee.

Wanawake walioko hapa ni akina mama, mabinti, na watoto wao. Hakuna mwanamume hata mmoja.

Baadhi ya wanawake hawa, waliwahi kupitia manyanyaso ya kijinsia ikiwemo kupigwa au hata kufukuzwa wakiwa na waume zao.

Wengine walishambuliwa na kubakwa walipokuwa wakichunga mifugo yao kama mbuzi na ng’ombe, au hata walipokuwa wakikusanya kuni.

“Hiki ni kijiji chetu kama wanawake,” mkazi mmoja anamwambia mwandishi wa makala hii, na kuongeza, “Hakuna mwanamume anayeruhusiwa kulala hapa. Hakuna mwanamume anayeishi hapa.”

Wengi wao walijikuta wameishia katika makazi haya, badala ya kupata msaada au kuhurumiwa kwa yale waliyopitia, ikiwemo kulaumiwa au kutengwa na jamii.

“Wakati mambo haya yanapotokea,” anaeleza Pauline Loldepe, Kiongozi na Mratibu wa Wanawake kijijini humo, “Wanasema sisi tulikuwa wazembe, wanatuona kama watu wasio na maana katika jamii. Ndiyo maana tulikuja hapa.”

Leo hii, kuna jumla ya wanawake 38 ambao wanaishi pamoja na watoto wao katika kijiji hicho, wote wanategemeana kwa usalama wao.

Kijiji kilivyojengwa

Kijiji hiki kilianza kama hifadhi na kimbilio la wanawake hawa, na pole pole kilibadilika na kuwa kijiji kamili.

Kwa umoja na ushirikiano wao, wanawake hawa wamefanikiwa kujenga nyumba nne aina ya manyatta ambazo zinatumika kuwapa hifadhi wakazi wa kijiji hicho.

Manyatta ni makazi ya kitamaduni ya jamii ya Wasamburu; manyatta moja huwa na takribani nyumba ndogo sita zilizojengwa katika eneo moja.

Wanaume ambao ni baba wa watoto wanaoishi na wanawake hawa wanaruhusiwa kuwatembelea watoto wao, lakini nje ya mipaka ya kijiji.

Mwanamke anaweza kuondoka kijijini ili kupata ujauzito na baadaye kurejea kijijini, ambapo hupata msaada unaofaa wakati wa ujauzito wake.

Usiku mmoja ndani ya kijiji cha wanawake

Kuwasili kwangu kunaleta hisia tofauti. Kwanza kabisa, natambulishwa kwa mratibu wa jamii, ambaye anaonekana kupendwa na kuheshimiwa kutokana na mapokezi ya kirafiki anayopata kutoka kwa kila mwanamke kijijini.

“Huyu anaitwa Kevin,” analiambia kundi lake la kina mama.

“Tumemkaribisha akae hapa usiku wa leo ili aone jinsi tunavyoishi. Tafadhali msimfukuze.”

Wanawake hao wanacheka, na baada ya majadiliano wanakubali ombi lake. Hivyo ninaruhusiwa kukaa, lakini kwa usiku mmoja tu, wanasema, chini ya uangalizi wao.

Ninalala peke yangu, juu ya sehemu iliyotengenezwa kwa ngozi ya mbuzi.

Ulikuwa ni usiku uliotulia, ambapo mara kwa mara nilisikia sauti za ving’ora. Ninalala bila usumbufu.

Asubuhi na mapema, niliamshwa na milio ya ndege na nyimbo za Kisamburu kutoka kwa wanawake walionikaribisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *