
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa ofisi hiyo, Jeremy Laurence, ametoa wito wa dharura kwa mamlaka za Iran kusitisha mara moja ukandamizaji wa kikatili dhidi ya raia wanaodai haki zao.
“Tunashtushwa na kuongezeka kwa ghasia zinazoelekezwa na vikosi vya usalama kwa waandamanaji kote nchini Iran, huku ripoti zikiashiria kuwa mamia wameuawa na maelfu kukamatwa,” amesema Laurence.
Umoja wa Mataifa umekosoa vikali mbinu ya serikali ya kuwabandika lebo ya “magaidi waandamanaji ili kuhalalisha matumizi ya nguvu”. Laurence amesisitiza kuwa mauaji ya waandamanaji wa amani lazima yakome na kutoa wito wa kurejeshwa kwa huduma za mawasiliano.
Ameongeza kuwa “Tunahimiza mamlaka za Iran kusitisha mara moja aina zote za ghasia na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wa amani na kurejesha upatikanaji kamili wa huduma za intaneti na mawasiliano.”
Historia inajirudia Katika hatua nyingine, Laurence amekumbusha kuwa hali ya sasa inafanana na ile ya mwaka 2022, ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kudai mabadiliko ya msingi.
Amesema kuwa hatua ya mamlaka kwa mara nyingine imekuwa ni kutumia nguvu kupita kiasi badala ya kusikiliza madai halali ya wananchi kwa ajili ya usawa na haki.
“Mzunguko huu wa ghasia za kutisha hauwezi kuendelea. Watu wa Iran na madai yao ya usawa na haki lazima yasikilizwe. Mauaji yote, ghasia dhidi ya waandamanaji, na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu lazima vichunguzwe kulingana na kanuni na viwango vya kimataifa, na wale waliohusika wawajibishwe,” amesisitiza.
Ripoti kutoka nchini humo zinaonesha kuwa hospitali kadhaa zimezidiwa na idadi kubwa ya majeruhi, wakiwemo watoto. Aidha, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, imeelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kutumika kwa hukumu ya kifo dhidi ya waandamanaji kupitia michakato ya haraka ya kimahakama.
Msemaji huyo amehitimisha kwa kusisitiza msimamo wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuwa Wairan wana haki ya kuandamana kwa amani na kwamba malalamiko yao yanapaswa kushughulikiwa badala ya kutumiwa kwa maslahi ya kisiasa.
