DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC Insurance), Kaimu Abdi Mkeyenge, ameongoza ujumbe wa NIC katika ziara rasmi iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambapo walipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Daniel Malanga.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa kuishirikisha TCAA kuhusu utekelezaji wa Bima ya Lazima ya Msafiri (Mandatory Inbound Travel Insurance), inayotekelezwa kwa mujibu wa kifungu cha 134A cha Sheria ya Bima, Sura ya 394, kama kilivyoongezwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 (The Finance Act, 2025).
Kwa mujibu wa kifungu hicho, kila mgeni anayeingia Tanzania Bara kupitia viwanja vya ndege, bandari au mipaka ya nchi kavu anatakiwa kuwa na bima halali ya safari itakayomlinda kwa kipindi cha hadi siku 92 tangu kuingia nchini.

Katika mkutano huo, pande zote mbili zilijadili namna bora ya kuratibu utekelezaji wa sheria hiyo kwa kushirikiana, hususan katika mifumo ya usafiri wa anga na taratibu za uingiaji nchini, ili kuhakikisha ufanisi, uwazi na urahisi kwa wasafiri wanaoingia nchini.

Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya bima na sekta ya usafiri wa anga katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wasafiri, pamoja na kuchangia ukuaji endelevu wa sekta ya utalii na usafiri kwa ujumla.