WAKAZI wa Dar es Salaam wana kila sababu ya kuanza kufurahia huduma za usafi ri, baada ya Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka (UDART) kubainisha kuwasili kwa mabasi mengine 50 ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), maarufu mwendokasi.

Imeelezwa kuwa, kuwasili kwa mabasi hayo kutoka China yanakamilisha idadi ya mabasi 100 yakiwa ni pamoja na 49 yaliyowasili wiki iliyopita na basi lingine moja lililofika Machi, mwaka jana kwa ajili ya kufanya majaribio.

Kwa mujibu wa Ofisa Mawasiliano na Masoko wa UDART, Gabriel Katang lengo ni kutimiza ahadi walizotoa awali tangu mwaka jana, kwamba wataleta mabasi 100 na serikali kuwezesha mchakato mzima wa kununua mabasi 100, hivyo idadi yake inakamilika kwa kuunganisha ya kwanza 49 yaliyokwishapokelewa na 50 yaliyotarajiwa kuwasili jana.

Ujio wa mabasi hayo mapya ya mwendokasi ni hatua muhimu katika kuboresha usafiri wa umma mijini. Mabasi haya yameleta nafuu kubwa kwa wananchi kwa kupunguza msongamano wa magari, kuokoa muda wa safari na kuongeza usalama pamoja na uhakika wa usafiri.

Tunaamini ni uwekezaji mkubwa wa fedha za umma unaolenga kuinua uchumi na kuboresha maisha ya watu wengi. Hata hivyo, mafanikio ya mradi huu hayataamuliwa na idadi ya mabasi au ubora wa miundombinu pekee, bali pia na namna sisi wananchi tutakavyoyatunza.

Mfano, matukio ya uharibifu wa makusudi, uchafuzi wa mabasi, wizi wa vifaa au kutotii sheria na taratibu za matumizi yanaweza kuurudisha nyuma mradi huu mzuri. SOMA: Latra: Nauli ya Sh 1,000/- mwendokasi ni ya mpito

Mabasi haya ni mali ya umma, yakiharibiwa ni sisi sote tunaoathirika kwa kukosa huduma bora na kubebeshwa gharama za matengenezo. Ni wajibu wa kila mwananchi kutumia mabasi ya mwendokasi kwa nidhamu na uadilifu, kulinda viti, milango na madirisha, kuepuka kutupa taka hovyo, kulipa nauli stahiki na kufuata maelekezo ya wahudumu.

Aidha, mamlaka husika ziendelee kutoa elimu kwa umma, kusimamia sheria na kuchukua hatua stahiki dhidi ya waharibifu ili kulinda uwekezaji huu. Kwa pamoja tukiwa na moyo wa uzalendo na uwajibikaji, tunaweza kuyatunza mabasi haya mapya ya mwendokasi na kuhakikisha yanatoa huduma bora kwa muda mrefu.

Rai yetu kwa wananchi kuwa wazalendo na uchungu wa kulinda vitu vya thamani vinavyotusaidia sisi wenyewe, kwani kutunza mali ya umma ni kuitunza kesho yetu. Wananchi tuyatunze mabasi ya mwendokasi, kwani ni yetu sote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *