SHINYANGA: SERIKALI haitataka kuona mwanafunzi yeyote anakaa chini wala kusomea nje sababu imetoa fedha nyingi za ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye upungufu wa vyumba hivyo na wanafunzi wanaoishi mbali wamejengewa shule shikizi kuwarahisishia.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu ambapo alisikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wa eneo hilo.

Mhita amesema kama kuna shule ambayo ina upungufu wa vyumba vya madarasa watoto wasisome wakiwa nje bali uwekwe utaratibu mzuri wa madarasa yaliyopo ili wote waenee kwenye madarasa wakati serikali inaendelea kujipanga zaidi.

“Kero niliyoipata hapa ni shule ya msingi Mkombozi watoto wanasoma wakiwa nje tena wanakaa chini mkurugenzi nakuagiza kama hakuna vyumba vya madarasa watafutiwe namna ya kusoma kwenye vyumba ikiwemo waongezwe kwenye madarasa mengine au wapelekewe kwenye shule shikizi”amesema Mhita.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hadija Kabojela amesema tayari kuna shilingi Milioni 40 za kutekeleza ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule hiyo na mkandarasi amekwisha patikana na ujenzi utaanza muda sio mrefu.

Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani aliyekuwepo kwenye mkutano huo wa hadhara amesema hivi sasa hakuna changamoto kubwa kama ilivyokuwa zamani eneo ambalo lilikuwa likikwamisha shughuli za maendeleo na wanafunzi kwenda shule yameemnda yakishughulikiwa na serikali upo mto uliokuwa ukijaa maji nakufanya wanafunzi kutopita sasa daraja limejengwa kwa shilingi bilioni nne.

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama Thomas Myonga amesema serikali imefanya kazi kubwa sana mabadiliko yameonekana kwa macho wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakipotosha wenzao kwa kuwalisha mataongo pori kila changamoto itatatuliwa kwa kutekeleza ilani ya chama.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kangeme waliohudhuria mkutano huo Deogratius Doto na Christina Fabian wameeleza kuwa shule ya msingi Mkombozi watoto wanasoma nje kutokana na vyumba vitatu vya madarasa kutokamilika waliiomba serikali kuwajengea vyumba hivyo haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *