Dar es Salaam. Mtoto wa kihuni. Kipisi cha mtu. Toka mitaa ya mandishi matatu. Namaanisha TMK. Said Fella, ila Gen Z wanamjua zaidi kwa jina la Mkubwa Fella. Huyo ndo ‘faunda’ wa Yamoto Band na wanamuziki kadhaa.
Ndiyo wale masela wa kitaa, wale ambao ‘long-taim’ kitambo hicho waliona Bongo michosho. Katika kusaka maisha wakaamua zao kujitosa nje ya mipaka ya Nyerere kwenda kusaka malisho bora.
Miaka ya 90, ilikuwa ni ‘fasheni’ ‘mablaza’ kuzamia kwa Madiba. Na tuliita kuzamia ‘kozi’ usafiri ulikuwa ni meli tu. Ukipitia njia za gari na ndege usingetoboa kwa makaburu. Wengi walirudishwa kindezi.
Waliita Bondeni au Kwa Madiba, wapo walioita Dizonga Kwa Natal. Na tulio wengi tuliita ‘Sauzi’. Yes! Huko ndo kulikuwa na michongo. Kabla ya wana kuanza kufunga mkanda na kupaa mambele sana kinyamwezi zaidi.
Wahuni wengi walipotelea Sauzi, wakiacha mitaa ya Kurasini, Keko, Tandika, Mtongani, Wailesi, Pire, Sokota, Sudan, Mburahati, Tabata, Kigogo, Mabibo, Ilala, Kino, Sinza, Mapipa mpaka Kiburugwa ikiwa na upweke wa wahuni.
Kila muhuni alizamia ‘Sauzi’ kwa sababu kule ilikuwa rahisi hata kupotelea kwa Pele (Braziliano). Watoto wa Mburahati Madoto, Kagera, Argentina, Tip Top hadi Mabibo Mpakani, Tandale, Kwa Ally Maua walitoweka.
Wapo waliorudi na kusepa tena na tena, na ambao hawakurudi tena Bongo. Walilowea ‘Sauzi’ na kutupwa jela, kubwia unga au kupigwa shaba na wahuni. Ujue Sauzi hadi leo bado kuna udwanzi mwingi kinaoma.
‘Blaza’ Fred, aliishi kota za mitaa ya Magomeni Usalama. Ambazo zilivunjwa na Jakaya na kujengwa ghorofa. Fred siyo tu aliiota Sauzi, hata jina alibadili kutoka Fred na kujiita Pietermaritzburg, jina la mji wa Kisauzi.
Miaka ya 90 maskani za wahuni stori zilikuwa na Kwa Zulu Natal tu. Wapo waliofia kwenye meli na waliopigwa shaba baada kufika. Na wapo waliotoboa maisha na kurudi Bongo wakiwa watamu kinoma.
Ukweli ni kwamba kuzamia meli ilikuwa ni hasara zaidi ya faida. Leo pisi kali kibao zinadondoka Sauzi kwa mwewe tu. ‘Laifu’ ya kudandia injini ya meli imebaki kuwa historia ya wahuni wa kale.
Fella ni mmoja wapo kati ya wale ‘wahuni’ waliozamia ‘Sauzi’. Pia ni mmoja ya wachache walioona Bongo kuna fursa zaidi. Alirudi zake Bongo na kuamua kupiga mishe hapa hapa mjini Daslama mpaka leo.
Wote watoto wa Tmk. Ikawa ni rahisi kukutana na ‘Necha’. Benzi ya kwanza ya ‘Necha’ ililetwa na Fella toka Dizonga. Ni Sir Nature tunayemuongelea akiwa katika ubora wake, nyakati ambazo kila agusacho kinageuka dhahabu.
Said Fella aliona fursa ndani ya muziki. Na Juma Nature aliona kitu ndani ya Said Fella. Pamoja wakawa marafiki wa faida, yule mwanamuziki huyu msimamizi wa kazi za muziki wake. Safari ikaanza.
Fella alimkuta Nature tayari akiwa maarufu. Lakini umaarufu wake ulikosa ‘propa menejimenti’. Yes! Akawa anaenda tu kwa mazoea kama wengine, kwa kiasi flan uwepo wa Fella ulibadili hali ya Kassim Kiroboto.
Ni miaka ile studio zinamiliki wasanii. Lakini wasanii walikosa usimamizi na hapo ndipo jina la Fella lilianza kuteka. Kuna mengi sana mazuri yalifanyika ambayo kabla ya Fella hayakuwepo kwa Nature.
Kama ambavyo leo ukiwa karibu na Diamond lazima ujulikane. Ni hali hiyo hiyo nyakati zile ukiwa ‘araundi’ Juma Nature ilikuwa ni lazima ujulikane. Jina la Said Fella likawa kubwa kwenye huu muziki.
Kabla baadaye hawajatengana. Katika kile Nature alilalamikia kuwa ‘anapunjwa’ anachostahili. Said Fella akabaki na Chegge na Temba, KR Mullah, Marehemu Y P pamoja na Y Dash na wengine.
Nature akasepa na Dolo, Rich One, Karama na kuungana na Inspekta Harun na wana kibao. Ndipo ikaibuka Wanaume Halisi na Wanaume Family. Ukweli ni kwamba Fella na vijana wake pia walisimama imara.
Lakini Fella alionesha ukubwa zaidi, pale alipokuja na Yamoto Band. Akiwa na Aslay na watoto wengine kina Mbosso, Enock Bella na Beka. Hii ilimfanya Fella kuwa mkubwa kweli kweli katika ‘indastri’ na kuheshimika.
Bila shaka hali hii pia ilipelekea Fella aaminike hata na Bosi Ruge. Pia ikawa rahisi kuaminika na Diamond. Kwa sababu Diamond alikuwa anamsikia Said Fella kwa miaka mingi, pengine akaona huyu atamfaa.
Kumfaa kwenye ujenzi wa himaya ya WCB. Kama haitoshi akaibeba nguvu ya Said Fella na Babu Tale. Kabla ya ujio wa Sallam Sk. Ndio, Diamond alichanga karata zake vizuri, himaya yake ikawa inazidi kuwa imara.
Fella akanogewa na Mondi, hata Tale akanogewa na Mondi pia. Tip Top ikasahaulika sawa sawa na Wanaume Family kupuuzwa. Mbaya zaidi hata Yamoto Band ikaanza kutawanyika. Asalaale… Mondi noma.
WCB ikawa taasisi kubwa sana, hapa Said Fella, pale Babu Tale na kule Sallam Sk. Huku Mond Bin Laden akisimama katikati yao. Na kuanza kuzitawanya himaya zote za zamani kwa akili mnemba bia kushitukiwa.
Ukubwa wa Mondi ukaenda sawa na ukubwa wa WCB. Miradi yake mingi ikaanza kuchipua. Sallam akipambana na vita za nje, Fella na Tale wakiwa bize na vita za ndani kwa ndani. Mondi akazidi kupaa juu zaidi.
Ukweli ni kwamba Fella alikuta Diamond tayari ana jina kubwa.. Na Diamond alikuta Said Fella na wenzake wapo vyema kimaisha. Hivyo walikutana ili watengeneze pesa zaidi na siyo njaa njaa. Yes, pata nipate.
Baadaye Mond akawa bize sana na miradi yake. Tale akawa bize na ubunge wake na Fella akawa bize na udiwani wake. Na Sallam Sk akawa bize na biashara zake. Lakini hili kamwe halikuondoa ukaribu wao.
Leo Said Fella anaumwa. Kelele ni nyingi mkewe anasema hivi, kwa Diamond wanasema lile na hili. Ila Mondi hajasikika akisema kitu, na Fella hajasikika akisema neno. Hii ni familia ya mitandao sana na hapo kabla ilikuwa ya magazeti.
Alamsik Bin Noor.