Chanzo cha picha, Ali Haj Suleiman/Getty Images
Serikali ya Syria imetangaza kusitishwa mara moja kwa mapigano kote nchini kati yake na Vikosi vinavyoongozwa na Wakurdi, (SDF) hatua inayoiwezesha serikali kudhibiti karibu nchi nzima, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Syria.
Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanamaliza takribani wiki mbili za mapigano makali na ni sehemu ya makubaliano mapana ya vipengele 14, ambayo yataifanya SDF kuunganishwa rasmi katika jeshi la Syria na taasisi za serikali.
Akizungumza mjini Damascus, Rais Ahmed al-Sharaa alisema makubaliano hayo yatawezesha taasisi za serikali ya Syria kurejesha mamlaka katika magavana (mikoa) mitatu ya mashariki na kaskazini, al-Hasakah, Deir Ezzor na Raqqa.
Hatua hiyo imefuatia mkutano kati ya Rais al-Sharaa na mjumbe maalum wa Marekani kwa Syria, Tom Barrack, uliofanyika Damascus. Barrack alisifu makubaliano hayo akisema ni hatua muhimu kuelekea “Syria iliyoungana.”
Kamanda wa SDF, Mazloum Abdi, alitarajiwa kuhudhuria mkutano huo lakini hakuwahi kusafiri kutokana na hali mbaya ya hewa, na ziara yake ikaahirishwa hadi Jumatatu, alisema Rais al-Sharaa.
Katika hotuba ya televisheni, Abdi alithibitisha kuwapo kwa mkutano huo na kusema kwamba atatoa maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo kwa Wakurdi wa Syria baada ya kurejea kutoka mji mkuu.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Kikurdi Ronahi, Abdi alisema makubaliano aliyofikia na Damascus yalijumuisha kusitishwa kwa mapigano ili kuepusha vita vikubwa zaidi, akisisitiza kuwa mapigano hayo “yalilazimishwa” dhidi ya SDF.
Vikosi vinavyoongozwa na Wakurdi vilianzisha utawala wao wa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, takribani miaka kumi iliyopita, kwa msaada mkubwa wa Marekani, ambayo iliwapa silaha na mafunzo SDF kama mshirika wake mkuu wa ndani katika mapambano dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu (ISIS).
Unaweza kusoma;