Takribani watu 39 wamepoteza maisha baada ya ajali iliyohusisha treni za mwendokasi kusini mwa Hispania, huku mamlaka zikionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Zaidi ya watu 30 wanatibiwa majeraha makubwa hospitalini, waziri wa uchukuzi wa nchi hiyo, Oscar Puente alisema. Tukio hilo lilitokea karibu na mji wa Adamuz, karibu na jiji la Cordoba, wakati treni ya mwendo kasi iliyokuwa ikisafiri kutoka Malaga hadi Madrid ilipoacha reli na kuvuka hadi kwenye njia nyingine, mwendeshaji wa mtandao wa reli Adif alisema.
Treni iliyoacha reli kisha ikagongana na treni nyingine ikisafiri kutoka Madrid kuelekea Huelva. Huduma za dharura za Andalusia zilisema takribani watu 73 walijeruhiwa katika ajali hiyo.
Tukio hilo lilionekana kuwa la ajabu sana, Puente aliongeza, kwa sababu treni iliacha njia moja kwa moja, ambayo ilikuwa imekarabatiwa Mei mwaka jana. Chanzo rasmi bado hakijajulikana. Uchunguzi kubaini kilichotokea utachukua takribani mwezi mmoja.
Waziri Mkuu, Pedro Sánchez, alisema nchi hiyo itapitia “usiku wa maumivu makali”. Iryo, kampuni binafsi ya reli iliyoendesha safari hiyo kutoka Malaga, ilisema takriban abiria 300 walikuwa ndani ya treni iliyoacha njia kwa mara ya kwanza, huku treni nyingine, inayoendeshwa na shirika la Renfe ikiwa na abiria wapatao 100.