Afrika Kusini imetangaza janga la kitaifa kutokana na mvua kubwa na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 30 kaskazini mwa nchi hiyo, kuharibu maelfu ya nyumba na kusomba barabara na madaraja.

Tamko hili limetolewa na Mkuu wa Kituo cha Ttaifa cha Kukabiliana na Maafa na Majanga ya Kimaumbile na kutangazwa na serikali.

Majimnbo yaliyoathiriwa pakubwa na mafuriko nchini Afrika Kusini ni Limpopo na Mpumalanga ambako watu wamepoteza maisha. 

Hata hivyo Wizara ya Uongozi wa Ushirika na Masuala ya Utamaduni imeeleza kuwa majimbo mengine yasiyopungua matatu pia yameathiriwa na hali mbaya ya hewa. 

Baadhi ya maeneo ya Afrika Kusini na nchi jirani za Msumbiji na Zimbabwe yamekumbwa na mvua kubwa kwa wiki kadhaa sasa. Mvua hizo zimesababisha   mafuriko makubwa katikati na kusini mwa Msumbiji, na kaskazini mwa Afrika Kusini.

Hadi sasa watu zaidi ya 100 wamefariki dunia katika nchi hizo tatu tangu mvua ianze kunyesha mwishoni mwa mwaka jana.

Mafuriko yaliyotokea kaskazini mwa Afrika Kusini yamepelekea kufungwa Hifadhi ya Taifa ya Kruger na kuhamishwa kwa mamia ya watalii na wafanyikazi kutoka kambi zilizofurika hadi sehemu zingine salama za mbuga hiyo.

Mkuu wa jimbo la Limpopo amesema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha uharibifu wa takriban dola milioni 240 katika jimbo lake, na nyumba nyingi na majengo yamesombwa na maji kikamilifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *