
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) Muhammad Baqer Qalibaf amesema kuwa “Vita vya kigaidi vya mtindo wa Daesh” vya hivi karibuni hapa nchini vilikuwa na malengo sawa na ya shambulio la kigaidi la Israel dhidi ya Lebanon mwezi Septemba mwaka 2024.
Septemba 17, 2024 maelfu ya maelfu ya vifaa vya mawasiliano visivyotumia waya vya wanachama wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon vililipuka kwa pamoja katika maeneo tofauti hukoLebanon na Syria, na kuua watu wasiopungua 12 na kuwajeruhi wengine karibu 3,000, wengi wao wakiwa raia wa kawaida.
Utawala haramu wa Israel ulitangaza rasmi kuhusika na mashambulizi hayo ya kigaidi.
Milipuko ya kiholela ya vifaa vya pager, iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, ilifuatiwa na mlipuko wa redio ya njia mbili ya kubeba mkononi siku iliyofuata, milipuko iliyojeruhi mamia ya watu.
Akizungumza bungeni leo Jumatatu, Qalibaf amesema: Njama hiyo iliyopangwa ilijumuisha ghasia na uharibifu wa wazi na ulioratibiwa, mashambulizi ya kigaidi na ya silaha mbalimbali, mauaji ya kikatili dhidi ya maelfu ya raia, vikosi vya Basij, polisi na vikosi vya usalalama.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Mkakati huo ulikusudiwa kuibua hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi ili washindwe kuchambua mambo na kuacha kuiunga mkono nchi; na katika mazingira hayo kutoa mwanya kwa Marekani na mamluki wake kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran na kuisambarisha nchi.
“Ni nchi chache duniani ambazo zinaweza kurejesha usalama haraka iwezekanavyo na kuwalinda watu wake baada ya kukabiliwa ghafla na “ugaidi uliopangwa na wa kikatili”, kwa uungaji mkono wawazi na rasmi wa Rais wa Marekani, amesema Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran.