Dar es Salaam. Mwanamuziki maarufu Akon, ameendelea kuwa funzo kwa mastaa wengi duniani, hii ni baada ya kuonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa taifa lake la Senegal.

Akon amekuwa mmoja wa mastaa ambao walifuatilia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kuanzia mwanzo hadi mwisho, ambapo zilianza Desemba 21, 2025 na kutamatika Januari 18, 2026.

Nyota huyo ambaye amewahi kufanya kazi na mastaa wakubwa duniani, alionekana mara kadhaa uwanjani akishiriki hisia zake kwa kuimba na kushangilia kama mashabiki wengine bila kujali umaarufu wake. Hatua hiyo iliwavutia na kuwashangaza wengi kwani mastaa kama yeye wamezoeleka kujitenga katika matukio kama hayo.

Katika mashindano hayo, Akon hakukosa hata mechi moja muhimu ya timu ya taifa ya Senegal ijulikanayo kama ‘Simba wa Teranga’, alianza kuonekana kuanzia hatua ya makundi hadi fainali ambapo Senegal ilifanikiwa kulibeba kombe hilo kwa mara ya pili katika historia yake.

Mashabiki mbalimbali waliotoa maoni yao katika mitandao ya kijamii wanasema kitendo cha Akon ni somo tosha kwa mastaa wengine wa Kiafrika na kimataifa. Ambao mara nyingi hujitenga na mataifa yao pindi wapatapo umaarufu. Huku wakimsifu Akon kwa kueleza kuwa uzalendo haukuwa wa maneno mitandaoni, bali wa vitendo, kuwa bega kwa bega na timu yake ya taifa.

Aidha baadhi ya mashabiki wanaeleza Akon ameonyesha kuwa umaarufu haupaswi kumfanya mtu aisahau mizizi yake. Badala yake, anatakiwa kutumia jina lake na ukubwa wake kuitangaza nchi yake, kuimarisha umoja wa kitaifa na kuwapa vijana motisha ya kuipenda nchi yao.

Ushindi wa Senegal katika AFCON 2025 haukuwa tu wa wachezaji na benchi la ufundi, bali ulikuwa ni wa wananchi na mashabiki walikuwepo akiwemo Akon ambaye alisimama kama raia wa kawaida mwenye mapenzi ya dhati kwa nchi yake.

Aidha, baada ya ushindi huo, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, Jumatatu, Januari 19, 2026, alitangaza kuwa sikukuu ya kitaifa ili kuenzi ushindi wa timu ya taifa kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Baada ya Senegal kushinda 1–0 dhidi ya Morocco katika mechi iliyofanyika Rabat nchini Morocco.

Hata hivyo, kikosi cha Senegal usiku jana kiliwasili jijini Dakar, na kupata mapokezi makubwa yaliyoongozwa na Rais Bassirou Diomaye Faye.

Akon ni nani?
Akon ni mwanamuziki, mtayarishaji wa muziki na mfanyabiashara maarufu wa kimataifa mwenye asili ya Senegal na Marekani.

Jina lake halisi ni Aliaune Damala Badara Akon Thiam, alizaliwa Aprili 16, 1973, St. Louis, Marekani. Baba yake, Mor Thiam, ni Msenegal halisi na mama yake ni Kinte Kaul, ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika (Mmarekani Mweusi).

Akon alianza kutambulika mwaka 2004 kupitia wimbo Locked Up, huku akipata umaarufu zaidi kupitia vibao kama Smack That, Lonely, Right Now (Na Na Na) na Don’t Matter. Mbali na kuimba, ameibua na kusimamia vya mastaa wakubwa akiwemo Lady Gaga.

Zaidi ya muziki, Akon anafahamika kwa miradi ya maendeleo barani Afrika, ukiwemo ‘Akon Lighting Africa’, mradi uliolenga kusambaza umeme wa jua katika nchi nyingi za Afrika, pamoja na wazo la Akon City nchini Senegal.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *