Dar es Salaam. mtandao wa kijamii uliotokea kupendwa na mastaa wengi Bongo na hata duniani kwa ujumla kama Instagram, baadhi unaweza kuwakosa katika mitandao yote mingine lakini sio Instagram.
Lakini hadi unawaona katika mtandao huo, kuna mengi ambayo huendelea nyuma ya pazia, wapo walioshawishiwa na wenzao kujiunga na wapo wenye rekodi za kipekee kama ifuatavyo:
1. Mwimbaji Ray C ndiye alimfungulia Mrisho Mpoto ukurasa (akaunti) wake wa Instagram ambao hadi sasa una wafuasi (followers) zaidi milioni moja tangu ufunguliwe Januari 2014.
2. Hata hivyo, Mwana FA (Hamisi Mwinjuma) ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiye alimshawisha sana Mpoto kujiunga kwenye mtandao huo.
3. Mchekeshaji wa kundi la Orijinal Comedy, Mpoki alipojiunga Instagram mnamo Julai 2016, mwanamuziki wa kwanza kumfuata (follower) ni rapa Fid Q kwa sababu yeye ni shabiki wake mkubwa.
4. Mpoki anaukubali sana uandishi wa Fid Q (Fareed Kubanda) katika nyimbo zake kwa mtindo wa kufikirisha na mpangilio mzuri wa vina, hivyo mtoto wake wa kwanza wa kiume alimpa jina la Fareed.
5. Mwimbaji kutokea Kings Music, Alikiba, ukurasa wa Instagram anaopenda kuufuatilia mara kwa mara ni wa klabu anayoishabikia katika Ligi Kuu England (EPL), Liverpool.
6. Baada ya Ben Pol kumwimba Salama Jabir (Ece Jay) katika wimbo wake, Jikubali (2013), ndipo mtangazaji huyo akamfuata (follow) Instagram akiwa ni mtu wa kwanza maarufu Bongo kufanya hivyo.
7. Hadi Desemba 2015, Diamond Platnumz alikuwa ndiye msanii mwenye wafuasi wengi Instagram Afrika akiwa nao milioni 1.5, lakini kufikia Septemba 2016 akashushwa na Davido aliyefikisha wafuasi milioni 2.9.
8. Akiwa tayari amejihusisha na uigizaji, mitindo, muziki na sasa akisimama kama mshawishi wa chapa mtandaoni, Hamisa Mobetto anajivunia kuwa staa wa kike mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram. Hamisa ambaye ni Miss XXL After School Bash 2012, amefikia rekodi hiyo baada ya kumpiku Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye aliongoza kwa muda mrefu.
9. Instagram ndio mtandao ambao Diamond ameutaja sana katika nyimbo zake, baadhi ya hizo ni Utanipenda (2015), African Beauty (2018), Inama (2018), Kanyaga (2019), Haunisumbui (2020), Wonder (2021) n.k.
10. Mwanamitindo wa kimataifa kutokea Bongo, Flaviana Matata, ndiye Mtanzania pekee ambaye mwimbaji maarufu wa Pop na R&B duniani, Rihanna amemfuata (follow) Instagram hadi sasa. Ndiyo, Rihanna yule wa nyimbo kali kama Diamonds (2012), Work (2016) na Umbrella (2007), naye ni miongoni mwa wanaziona kwa ukaribu na haraka posti kutoka kwa Flaviana, Miss Universe Tanzania 2007.