
Benyamin Netanyahu amekubali mwaliko kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump wa kujiunga na “Baraza lake la Amani,” ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imetangaza leo Jumatano, Januari 21.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ofisi ya Benyamin Netanyahu imetangaza Jumatano kwamba Waziri Mkuu wa Israeli amekubali kujiunga na “Baraza la Amani” la Rais wa Marekani Donald Trump, huku Sweden ikikataa mwaliko huo na, kulingana na vyombo vya habari vya Italia, Roma inatarajiwa kufanya vivyo hivyo.
Mialiko ilitumwa kwa angalau nchi sitini, lakini mbali na Israel, ni chache tu, ikiwa ni pamoja na Hungary, Azerbaijan, Armenia, Kazakhstani, Kosovo, Falme za Kiarabu, na Misri, hadi sasa zimekubali hadharani kushiriki katika mpango huu.
“Benjamin Netanyahu amekubali mwaliko kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump wa kujiunga, kama mwanachama, na ‘Baraza la Amani,’ ambalo litaundwa na viongozi kutoka nchi kote ulimwenguni,” kulingana na taarifa fupi kutoka ofisi yake iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP.
Norway haitashiriki katika “Baraza la Amani” la Trump
Norway, ambayo uhusiano wake umezorota sana na Donald Trump, ambaye alikasirika kwa kutopokea Tuzo ya Amani ya Nobel, haitashiriki katika “Baraza la Amani” lililopendekezwa na rais wa Marekani, ofisi ya Waziri Mkuu imetangaza leo Jumatano. “Pendekezo hilo la Marekani linaibua maswali kadhaa ambayo yanahitaji mazungumzo zaidi na Marekani. Kwa hivyo Norway haitajiunga na mipango iliyopendekezwa ya Baraza la Amani na haitashiriki katika sherehe ya utiaji saini huko Davos,” amesema waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu, Kristoffer Thoner katika ujumbe kwa AFP.
China inasema inatetea mfumo wa kimataifa unaozingatia Umoja wa Mataifa
China ambayo imealikwa kujiunga na “Baraza la Amani” la Trump, imesema leo Jumatano inatetea mfumo wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa, baada ya kutangaza siku iliyopita kwamba imealikwa kujiunga na “Baraza la Amani” lililopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump. Siku ya Jumanne Januri 20, Beijing ilisema kwamba imealikwa na Marekani kushiriki katika “Baraza hili la Amani,” linalokusudiwa kufanya kazi katika kutatua migogoro duniani kote na kuonekana sana kama mpinzani wa Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alijizuia kusema leo Jumatano kama China itakubali mwaliko huo. Lakini, msemaji huyu, Guo Jiakun, amesema wakati wa mkutano wa kila siku na waandishi wa habari, “bila kujali mabadiliko katika hali ya kimataifa, China inatetea kwa dhati mfumo wa kimataifa pamoja na Umoja wa Mataifa, utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria za kimataifa, na sheria za msingi za mahusiano ya kimataifa zinazozingatia madhumuni na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”