
Mwandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa nchini Msumbiji, Ouri Pota, mapema leo ametuma taarifa ikieleza kwamba serikali ya Msumbiji imetoa takwimu zikionesha mafuriko yamesambaratisha takriban nyumba 5,000, nyumba 82,000 zimejaa maji, na vituo vya afya 56 vimethirika tangu kuanza kwa msimu wa mvua ambao umeikumba nchi hiyo na mbaya zaidi takriban watu 120 wamefariki dunia, sita hawajulikani walipo, na 99 wamejeruhiwa.
Msemaji wa Serikali ya Msumbiji, Inocêncio Impissa akieleza changamoto wanazokumbana nazo katika kusaidia watu ameeleza kuwa bajeti iliyoidhinishwa hapo awali haikidhi mahitaji ya wale walioathiriwa na hali hiyo mbaya ya hewa, anasema, “bado tunahitaji kuimarishwa kwa bajeti ya takribani dola za Marekani bilioni 6.6 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Msumbiji, hasa wale waliokimbia makazi yao. Msaada huu utaimarisha misaada ya kijamii katika maeneo ya afya, chakula, na aina mbalimbali za misaada tunayohitaji kutoa katika awamu hii muhimu ya makazi, ili waweze kuwa sawa ipasavyo.”
Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama kawaida yamekuwa yakipambana kwa kila namna kusaidia wananchi wa Msumbiji kutoka katika hali hiyo tete ingawa hali ya kifedha nay oni tete kwa mashirika hayo. Mathalani shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), likieleza hali ya sasa ilivyo limesema janga la sasa nchini Msumbiji linazidisha zaidi udhaifu uliokuwepo hapo awali uliosababishwa na vimbunga vya Chido na Dikeledi mwaka jana 2025 na kiafya kujaa kwa maji kila sehemu kunazidisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea.
Shirika hilo linasema kwa upande wake, angalau dola za Marekani milioni 11.5 zinahitajika ili kuchukua hatua za kibinadamu, lakini ni asilimia 6 tu ya fedha hizo zinazohitajika zimekusanywa, na hivyo kuacha pengo kubwa.