Waandishi wa ripoti hiyo wanasema kuwa istilahi kama “msongo wa maji au mgogoro wa maji” hazielezei tena ipasavyo kinachoendelea katika maeneo mengi ya dunia.
Badala yake, wanabainisha hali ya baada ya mgogoro inayojulikana kwa upotevu wa kudumu wa mtaji wa asili wa maji.
Maeneo mengi hayana maji ya kutosha
“Ripoti hii inafichua ukweli usiofurahisha, maeneo mengi yanaishi zaidi ya uwezo wao wa hidrologia, na mifumo mingi muhimu ya maji tayari inashindwa,” amesema mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, Kaveh Madani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Maji, Mazingira na Afya ya Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa.
Nchi nyingi hazijatumia tu rasilimali zao za maji ikiwemo maji ya mito, maji yaliyomo kwenye udongo, na akiba ya theluji bali pia zimepunguza akiba ya muda mrefu ya maji kama vile barafu za milele na maeneo oevu.
Hali hii imesababisha madhara makubwa, yakiwemo kushuka kwa ardhi katika delta za mito na miji ya pwani, kutoweka kwa maziwa na maeneo oevu, na upotevu usioweza kurekebishwa wa bioanuwai.
Mashirika kama UN Water yanasaidia kuhakikisha kwamba watu duniani kote, ikiwa ni pamoja na Guatemala, (pichani) wanapata maji salama.r
Mkutano wa maji na ushirikiano wa kimataifa
Ripoti hii imetolewa kabla ya mkutano wa ngazi ya juu utakaofanyika Dakar, Senegal, tarehe 26–27 Januari, kama maandalizi ya Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa wa 2026, utakaofanyika tarehe 2–4 Desemba 2026 katika Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu UAE.
Ingawa si kila bonde la mto au kila nchi iko katika hali ya kufilisika kwa maji, Madani amesisitiza kuwa mifumo mingi muhimu ya maji duniani tayari imevuka kiwango hicho.
“Mifumo hii imeunganishwa kupitia biashara, watu kuhama makwao, mabadiliko ya tabianchi, na utegemezi wa kijiografia na kisiasa, hivyo kimsingi taswira ya hatari duniani imebadilika,” amesema, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika eneo hili.
Maeneo hatarishi
Kwa mujibu wa waandishi wa ripoti, hali Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ni mbaya sana kwani wanakabiliwa na uhaba wa maji, mishtuko ya tabianchi, uzalishaji mdogo wa kilimo, na dhoruba za mchanga.
Mabadiliko ya tabianchi, mawimbi ya joto na ukame unaoambatana nayo, yanazidisha tatizo la uhaba wa maji.
Katika baadhi ya maeneo ya Asia Kusini, shughuli za kilimo zinazotegemea matumizi makubwa ya maji ya chini ya ardhi na ukuaji wa miji zimesababisha kupungua kwa muda mrefu kwa viwango vya maji ya chini ya ardhi na kushuka kwa udongo katika maeneo fulani.
Katika maeneo ya kusini-magharibi mwa Marekani, Mto Colorado umekuwa ishara ya mgogoro wa maji unaosababishwa na matumizi kupita kiasi, mabadiliko ya tabianchi, na ukame unaohusiana nayo.
Takwimu za kufilisika kwa maji
Kwa kutumia takwimu za kimataifa na tafiti za hivi karibuni za kisayansi, ripoti inaonesha picha nzito ya mwenendo, ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na shughuli za binadamu:
- Asilimia 50 ya maziwa makubwa duniani yamepoteza sehemu ya ujazo wa maji tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990,
- Eneo la maeneo oevu ya asili yaliyopotea katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ni ekari milioni 410 (sawa na ukubwa wa Muungano wa Ulaya),
- Zaidi ya asilimia 30 ya uzito wa barafu za dunia umepotea tangu mwaka 1970, safu nzima za milima katika maeneo ya latitudo za chini na za kati huenda zikakosa kabisa barafu zinazofanya kazi katika miongo ijayo,
- Mito mikubwa kadhaa haifiki tena baharini katika vipindi fulani vya mwaka,
- Watu bilioni 4 hupitia uhaba mkubwa wa maji angalau mwezi mmoja kwa mwaka,
- Watu bilioni 3 wanaishi katika maeneo ambako upatikanaji wa maji kwa ujumla unapungua, ilhali maeneo hayo hayo huzalisha zaidi ya asilimia 50 ya chakula cha dunia,
- Watu bilioni 1.8 waliishi katika hali ya ukame katika kipindi cha 2022–2023.
Picha ya angani inayoonyesha mto Juba uliokauka nchini Somalia. Ukame wa muda mrefu kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa huathiri mamilioni ya watu katika eneo la Pembe ya Afrika.
Utambuzi mpya kwa enzi mpya
Kufilisika kwa maji ni jambo la kimataifa, waandishi wa ripoti wanasisitiza.
“Kilimo hutumia sehemu kubwa ya maji safi, na mifumo ya chakula imeunganishwa kwa karibu kupitia biashara na bei,” ameeleza Madani.
“Wakati uhaba wa maji unapodhoofisha kilimo katika eneo moja, athari zake husambaa katika masoko ya dunia, uthabiti wa kisiasa na uhakika wa chakula katika maeneo mengine,” ameongeza.
Wito wa kuweka upya ajenda ya maji duniani
Ripoti inaonesha kuwa kufilisika kwa maji si tatizo la hidrologia pekee, bali pia ni suala la usawa lenye athari kubwa za kijamii na kisiasa, linalohitaji kuangaliwa katika ngazi za juu zaidi za serikali na kupitia ushirikiano wa kimataifa.
“Hatuwezi kurejesha barafu zilizotowek lakini tunaweza kuzuia upotevu zaidi wa mtaji wa asili uliosalia na kujenga upya taasisi ili kukabiliana na hali mpya,” amesema Madani.
Matukio yajayo, yakiwemo Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa wa 2026, yanatoa fursa za kusukuma mbele ajenda hii.
Ripoti iliyotolewa leo ni wito wa mabadiliko amesema Madani akisistiza kuwa “Kwa kutambua uhalisia wa kufilisika kwa maji, tunaweza hatimaye kufanya maamuzi magumu yatakayolinda watu, uchumi na mifumo ikolojia. Kadri tunavyoendelea kuchelewa, ndivyo uhaba wa maji unavyozidi kuongezeka”.