
Wakati mkutano wa pili wa mazingira wa Afrika ukiendelea jijini Addis Ababa Ethiopia, wadau na wataalam wa nishati mbadala wanasubiri kuona ikiwa lengo lililoafikiwa katika mkutano wa kwanza jijini Nairobi mwaka 2023, la bara hilo kufikia uzalishaji wa gigawati 300 ya nishati mbadala kufikia 2030, litakuwa na matokeo chanya.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wataalam wa masula ya nishati wanasema Afrika ina uwezo wa kujifadhili licha ya upungufu wa ufadhili unaohitajika kuiwezesha kuondokana na matumizi ya nishati chafu.
Dkt Jessica Omukuti, ni mtafiti kutoka chuo kikuu cha Oxford.
“Nafikiri kuwa bara hili lina uwezo wa kujifadhili, kuna fursa kwenye rasilimali katika mataifa yanayoendelea kuokoa rasilimali kufadhili miradi ya nishati mbadala.” Amesema Dkt Jessica Omukuti.
Aidha, anasema changamoto nyingine ni mataifa kutokuwa na msimamo, kuhusu suala la kuachana na mafuta ya kisukuku kwa misimgi kuwa yana haki ya namna ya kutumia rasilimali zake.
“Ni hali ambayo mataifa yanaweza kujikwamua, kuna utashi wa kisiasa ambao unaweza kupelekea hatua zaidi kuchukuliwa ili kufanikisha mataifa kugeukia nishati mbadala.” alieleza Dkt Jessica Omukuti
Vijana ambao ndio asilimia kubwa ya nguvu kazi barani Afrika, nao wanazitaka serikali zao kuzingatia ufadhili wa miradi inayotoa ajira ya kijani. Rahma ni mwanamazingira kutoka Tanzania.
“Changamoto kubwa ambayo tunaipata kwenye ugawaji wa fedha ambazo zinatoka serikalini kwa hivyo tunataka serikali itusaidie kuwekeza kwa vitu tunavyofanya.” Alisema Rahma mwanamazingira kutoka Tanzania.
Kwa jumla mataifa ya Afrika yanahitaji kiwango cha kati ya dola trilioni 1.6 na trilioni 1.9 kufikia 2030 ili kuziwezesha kuachana na matumizi ya mafuta ya kisukuku.