Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amerudishwa tena mahabusu baada ya kesi yake ya uhaini kuahirishwa kwa mara nyingine.

Katika kikao cha leo, Lissu alipata nafasi ya kuwasilisha maelezo yake ya awali, yaliyolenga kuonyesha tofauti zilizojitokeza katika nyaraka za mahakama. Hali hiyo ilizua mvutano mkali kati yake na mawakili wa serikali.

Katika hoja zake, Lissu alisema nyaraka zilizotolewa na Mahakama zinapingana na hivyo kusababisha mkanganyiko. Akimalizia maelezo yake, alisema na hapa namnukuu:

“Na kama itawapendeza, mtoe amri kwamba hakukuwa na committal na mfute kila kilichopo, ili leo na mimi nikalale nyumbani kwangu baada ya kushikiliwa kwa siku zaidi ya 150 gerezani.” Mwisho wa kunukuu.

Kiongozi wa upinzani Tanzania apandishwa tena kizimbani

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Tofauti na jana, leo ukumbi wa mahakama ulikuwa umejaa watu wanaodaiwa kuwa polisi, jambo lililolalamikiwa na viongozi na wafuasi wa Chadema kuwa linawanyima nafasi ya kufuatilia kesi ya kiongozi wao.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, alitoa malalamiko kuhusu madai hayo ya polisi kujaza Ukumbi Namba 2 wa mahakama hiyo. Hakimu Dunstan Nduguru, baada ya kusikiliza majibu ya upande wa Jamhuri, aliahirisha kesi hiyo hadi kesho saa tatu kamili asubuhi, ambapo Lissu anatarajiwa kurejea tena kizimbani kwa muendelezo wa shauri hilo, baada ya kushindwa kumalizika leo kutokana na changamoto ya muda wa mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *