
Tukio hilo limeibua hofu na hasira miongoni mwa jamii, likichukuliwa kama ishara ya wazi ya chuki dhidi ya Waislamu.
Mkuu wa polisi wa Paris, Laurent Nunez, ameonya kwamba kuna uwezekano wa vichwa vingine zaidi vya nguruwe vikapatikana, akisisitiza kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba kila juhudi zinafanyika kuwasaka wahusika wa vitendo hivyo vya chuki.
Kwa mujibu wa mamlaka za mitaa, vichwa hivyo vilitupwa barabarani katika maeneo ya Paris na vitongoji vitatu jirani.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bruno Retailleau amelaani tukio hilo na kulitaja kuwa “kitendo cha fedheha na kisichokubalika kabisa.” Ameeleza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya kuchochea chuki na mgawanyiko wa kijamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Ulaya la Haki za Msingi, kumekuwepo na ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu na Wayahudi katika nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya tangu kuanza kwa vita katika ukanda wa Gaza mnamo Oktoba, mwaka 2023.