
Mkuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria wa Global Funds, Peter Sands amesema vifo vinavyotokana na ugonjwa malaria huenda vikaongezeka zaidi mwaka huu kutokana na kupunguzwa kwa misaada.
Itakumbukwa tangu aliporejea madarakani mwezi Januari, Rais wa Donald Trump wa Marekani alitangaza kusitisha misaada kwa mashirika ya kimataifa na tangu wakati huo bajeti za misaada ya maendeleo imezorota.
Marekani ndio iliyokuwa mfadhili mkuu wa shirika la Afya duniani WHO. Malaria, ambayo huenezwa na aina fulani za mbu, husababisha vifo vinavyokadiriwa kufikia 600,000 kwa mwaka, huku wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wakiwa waathirika wakubwa.
Kwa mujibu wa Sands ni kwamba kupungua kwa misaada hiyo huenda mwaka huu wa 2025 ukashuhudia ongezeko la vifo 100,000 zaidi huku bara la Afrika likitajwa kuwa katika hali mbaya zaidi.