Mgogoro huo uliochochewa na marufuku yenye utata kwenye mitandao ya kijamii, umeiacha Kathmandu chini ya amri ya kutotoka nje, huku maduka na shule yakuwa yamefungwa, na askari wakishika doria katika mitaa iliyochomwa moto.
Mazungumzo hayo yanafuatia maandamano yaliyoongozwa na kundi la vijana maarufu kama Gen Z na kuratibiwa kwa kiasi kikubwa kupitia mitandao ya kijamii ambapo yaliongezeka na kuwa ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, huku majengo ya serikali, hoteli na makaazi ya watu yakiteketezwa kwa moto.
Kundi la vijana waandamaji katika mazungumzo hayo wameweka masharti yao yenye vigezo vya kukidhi matakwa yao kufuatia hasira walizokuwa nazo dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu K.P. Sharma ambaye pamoja na uamuzi wa kuachia ngazi bado hakukupunguza gadhabu za waandamanaji waliooongeza shinikizo la kudai mabadiliko ya kimfumo na kupatikana kwa kiongozi mwadilifu wa kuiongoza taifa hilo.
Gen Z washinikiza mabadiliko ya kisiasa na uwajibikaji wa serikali
Tayari Jaji Mkuu wa zamani Sushila Karki ambaye ni mwanamke wa kwanza wa Nepal kushikilia wadhifa huo, ameibukana kutangaza nia yake ya kuwania nafasi ya kuwa waziri mkuu wa mpito, lakini maafisa wa jeshi na waandamanaji bado wanajadili njia ya kikatiba ya kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo.
Uamuzi wa Jaji Karki ulipokelewa kwa shangwe na baadhi ya vijana jana Jumatano usiku mara baada ya mwakilishi wa Gen Z, Rehan Raj Dangal kutangaza nje ya makao makuu ya Jeshi la Nepal kwamba waandamanaji walikuwa wakimpendekeza Karki kama waziri mkuu wa muda.
Taarifa za ndani zinasema kugombea kwake kunaungwa mkono na duru za kisheria, mashirika ya kiraia, na baadhi ya wanasiasa, ingawa migawanyiko imesalia ndani ya makundi ya waandamanaji na vyama vikuu vya kisiasa nchini humo.
”Miongoni mwa watu waadilifu na wasio na upendeleo wanaotambulika na umma, tumempendekeza kwa kauli moja Bi. Sushila Karki kuunda serikali ya mpito.”
Nia hii ya Karki kuliongoza taifa hilo kipindi cha mpito pamoja na kuungwa mkono na vijana wengi waandamajani, imekutana na pingamizi kutoka kwa baadhi yao wanaotilia shaka uwezo na dhamira ya Karki kuwakilisha matarajio ya kizazi kipya cha Nepal, kama anavyofafanua Mahendra Khadka, mmoja wa waandamanaji vijana.
“Mtazamo wetu ni kwamba hisia za umma na hisia za Gen Z hazipaswi kuchezewa, na ingawa kuna wagombea bora kuliko Sushila Karki, hatutamkubali Shusila Karki.”
Jeshi la Nepal ambalo katika kudhibiti madhara ya maandamano nchini humo liliamua kuongeza muda wa kutotoka nje kwa nchi nzima hadi Ijumaa, linasema kuwa linapatanisha mazungumzo ili kuzuia umwagaji zaidi wa damu na kurejesha utulivu nchini humo, huku vizuizi vilivyokuwa vimewekwa maeneo mbalimbali vikiwa vimepunguzwa kidogo kwa wafanyakazi muhimu na wasafiri wa ndege, ingawa maagizo ya marufuku yamesalia katika sehemu kubwa ya Kathmandu.
Kulingana na vyanzo vya hospitali na polisi, idadi ya majeruhi inaendelea kuongezeka, huku watu 35 wakiripotiwa kupoteza maisha na zaidi ya 1,000 kujeruhiwa.
Wafungwa tisa pia waliuawa katika majaribio ya kuvunja gereza huku vurugu zikienea katika mfumo wa magereza.
Kwa waandamanaji wengi, uteuzi wa Karki ni ishara ya matarajio yao ya uongozi wa uadilifu na uwajibikaji. Lakini kwa vile mgawanyiko bado upo, mustakabali wa kisiasa wa Nepal unabaki kuwa na mashaka huku jeshi likijaribu kuunganisha mapengo kati ya vijana waandamanaji, wanasiasa na taifa lililo katika mzozo.