
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imeilaani ile iliyoiita “kauli ya kipuuzi” ya Netanyahu, ambaye alikuwa amesema kuwa lazima Qatar iwafukuze au iwashitaki wale aliowaita ‘magaidi, ama Israel itafanya hivyo.
Doha imeyaita matamshi hayo kuwa vitisho vya wazi vya uvunjaji wa mamlaka ya taifa hilo la Ghuba, na jaribio la aibu kuhalalisha mashambulizi ya aibu yaliyofanywa na Tel Aviv nchini Qatar siku ya Jumanne (Septemba 9).
Jeshi la Israel liliwauwa watu sita kwenye mashambulizi ya kushangaza dhidi ya eneo lenye makaazi ya watu mjini Doha, likidai kuwalenga viongozi wa Hamas.
Miongoni mwa waliouawa ni mtoto wa kiume wa kiongozi wa Hamas, Khalil al-Hayya.
Mashambulizi hayo yamekosolewa vikali na viongozi mbalimbali ulimwenguni.