Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi, ameituhumu Rwanda kwa kuchelewesha utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Washington mwezi Juni, akisema Kigali inaendelea kushirikiana na waasi wa M23 licha ya madai ya kujiondoa.
Akizungumza pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Tshisekedi alisema Rwanda “inafanya hila za kununua muda ili hali iwe mbaya zaidi,” huku akisisitiza kuwa Kinshasa iko tayari kwa amani.
Kauli yake inakuja katika kipindi ambacho Kongo Mashariki imeendelea kushuhudia machafuko ya muda mrefu yanayohusisha makundi ya waasi, mara nyingi yakiwa na uhusiano na uporaji wa rasilimali adimu zinazopatikana katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani tarehe 27 Juni, Rwanda na Kongo ziliahidi kushirikiana kumaliza msaada kwa kundi la M23, ambalo Washington na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema limekuwa likifadhiliwa na Kigali.
Amani na rasilimali za madini
Rais Tshisekedi alimshukuru Rais wa Marekani Donald Trump kwa jitihada za kusaka suluhu ya kudumu, lakini akaonya kuwa hilo halimaanishi DRC “itaweka madini yake rehani.” Alitaja rasilimali kama cobalt, shaba na dhahabu kuwa nguzo ya maendeleo ya taifa lake.
Aidha, alifafanua kuwa ushirikiano wa kimkakati unalenga kuendeleza sekta ya madini, kuongeza thamani kupitia mnyororo wa uzalishaji na kuboresha miundombinu, hususan ya nishati, ili kuchochea uwekezaji wa kigeni na maendeleo ya kijamii.
Kongo Mashariki imeendelea kukumbwa na mapigano tangu M23 walipobeba silaha upya mwishoni mwa mwaka 2021. Tangu wakati huo, waasi hao wameteka maeneo makubwa na hata kuanzisha tawala zao katika miji ya Goma na Bukavu.
Kwa mujibu wa Kinshasa, mafanikio ya mkataba wa Washington yatategemea Rwanda kuacha mara moja msaada wake kwa waasi hao. Kigali, hata hivyo, imekanusha tuhuma hizo, ikidai kuwa jeshi lake linachukua hatua za kujihami pekee.
Diplomasia ya Qatar na mazungumzo yaliyokwama
Mnamo Machi, Qatar iliwezesha mkutano wa ghafla kati ya Tshisekedi na Rais Paul Kagame ambapo walitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano. Hatua hiyo ilitoa nafasi kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Kinshasa na M23.
Hata hivyo, mazungumzo hayo yalikwama baada ya pande hizo kushindwa kutimiza makubaliano ya tarehe 18 Agosti yaliyokusudia kusaini mkataba wa kudumu wa amani. Tofauti kubwa zilibaki kuhusu masharti ya awali.
Moja ya vikwazo vikuu ni suala la wafungwa. M23 inataka waasi wake walioko gerezani waachiliwe kabla ya makubaliano kusainiwa, lakini Kinshasa inasisitiza kwamba kuachiliwa kwao kutatokea tu baada ya kufikiwa kwa makubaliano kamili.
Tshisekedi, hata hivyo, alisema kuna maendeleo ya awali katika mpango wa kubadilishana wafungwa na kwamba serikali yake inasubiri ruhusa rasmi kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu kuanza utekelezaji wa mchakato huo.
Chanzo: AFP,Reuters
