
Umoja wa Mataifa (AFP) – Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba siku ya Jumanne, Septemba 23, katika Umoja wa Mataifa, ametangaza kwamba Tokyo kulitambua taifa la Palestina ni suala la muda tu, akielezea “kukasirishwa” kwake na maoni ya hivi karibuni ya maafisa wa Israel.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Nimekerwa sana na kauli za maafisa wakuu wa serikali ya Israel ambao wanaonekana kukataa kabisa wazo lenyewe la kujenga taifa la Palestina,” amesema Shigeru Ishiba. “Kwa nchi yetu, swali sio kama kutambua taifa la Palestina, lakini lini. Hatua zinazoendelea za serikali ya Israel za upande mmoja hazikubaliki,” ameongeza. “Nataka kuweka wazi kwamba ikiwa hatua zaidi zitazuia kufikiwa kwa suluhisho la serikali mbili, Japan italazimika kuchukua hatua zaidi kujibu,” Waziri Mkuu wa Japan amebainisha.
Wimbi la hivi majuzi la kutambuliwa linakuja huku kukiwa na ongezeko la ghasia katika Ukingo wa Magharibi, ambapo serikali ya Israel haijaficha nia yake ya kutaka kulitwaa eneo la Palestina, na siku chache tu baada ya kuanza kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi ya Israel katika mji wa Gaza. Kwa upande wake, Rais wa Marekani, Donald Trump aliona kwamba kutambua taifa la Palestina kutakuwa “tuzo” kwa “ukatili” unaofanywa na Hamas, akimaanisha shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa na kundi hilo la wanamgambo wa Palestina mnamo Oktoba 7, 2023, nchini Israel, ambalo lilianzisha vita katika Ukanda wa Gaza. Japan, mwanachama wa G7, ni mshirika wa karibu wa Marekani. Kwingineko barani Asia, Korea Kusini na Singapore zimekataa kuitambua Palestina kama taifa.
“Ugaidi unaosababishwa na Hamas na uharibifu huko Gaza ambao tunashuhudia leo umewahuzunisha watu wengi,” Bw. Ishiba pia amesema wakati wa hotuba yake huko New York. Kwake yeye, “kile muhimu zaidi ni kwamba Palestina inaweza kuwepo kwa njia endelevu, kuishi pamoja kwa amani na Israel.” “Tunatoa wito kwa Palestina kuchukua jukumu lake kama mwanachama anayewajibika wa jumuiya ya kimataifa.” Upande wa Palestina lazima uanzishe mfumo wa utawala unaohakikisha uwajibikaji,” ameongeza.
Ufaransa na nchi nyingine kadhaa, zikiwemo Uingereza na Canada, zilitangaza kulitambua ” taifa la Palestina” siku ya Jumatatu, zikijaribu kuongeza shinikizo kwa Israel kumaliza vita vyake vya takriban miaka miwili na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Takriban mataifa 150 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa sasa yanatambua taifa la Palestina, kulingana na hesabu ya shirika la habari la AFP.
© 2025 AFP