
Vikosi vya Israel vimewauwa takribani Wapalestina 15 hivi leo wakati viliposhambulia maeneo yaliyolenga nyumba na mahema huko Gaza, hayo yamesemwa na msemaji wa shirika la ulinzi wa kiraia katika eneo hilo alipozungumza na shirika la habari la AFP.
Mashambulizi hayo ya Israel ni mwendelezo wa operesheni yake ya kijeshi ya angani na ardhini kwenye mji wa Gaza na ambayo imewalazimu maelfu ya watu kuondoka katika maeneo hayo yenye idadi kubwa ya watu.
Mashambulizi hayo huko Gaza yanafanyika wakati uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ukiishutumu Israel kwa kufanya “mauaji ya halaiki” katika Ukanda wa Gaza, ukisema Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wakuu ndio waliochochea uhalifu huo.
Israel kwa upande wake imeyatupilia mbali matokeo hayo na kusema kwamba uchunguzi huo ni “uongo na potofu” licha ya madai kwamba sehemu kubwa ya maeneo ya Gaza imeharibiwa na vita na watu wake wanakabiliwa na njaa.