
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema itaunga mkono uamuzi wowote wa watu wa Palestina na Muqawama kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano Gaza linaloungwa mkono na Marekani, huku ikiionya jamii ya kimataifa kuhusu mwelekeo hatari wa mpango huo na historia ya kutokuwa na muamana Israel.
Katika taarifa yake, wizara hiyo imesema siku zote Iran imekuwa ikiunga mkono mipango inayolenga kusitisha uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, na kuhakikisha Wapalestina wanajitawala, ikinukuu Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948, na wajibu wa kisheria na kimaadili wa mataifa kuunga mkono mapambano halali ya Wapalestina.
Taarifa hiyo imeeleza bayana kwamba, maamuzi juu ya usitishaji vita wowote au suluhu ya kisiasa lazima yawe ya Wapalestina wenyewe, ikiwa ni pamoja na mrengo wa Muqawama.
Imesema Tehran inakaribisha uamuzi wao wowote unaohusu kusimamisha mauaji ya halaiki ya Wapalestina, kuondolewa kwa jeshi la Kizayuni linaloikalia kwa mabavu Gaza, kuheshimu haki ya watu wa Palestina ya kujitawala, kuruhusiwa kuingia kwa misaada ya kibinadamu Gaza na kulijenga upya eneo hilo lililozingirwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imeonya kwamba, kusitishwa kwa uhasama hakutawafanya wahusika wa kimataifa kuachana na wajibu wao wa kutafuta uwajibikaji wa kisheria.
Wizara hiyo imesisitiza kuwa, kusitishwa kwa vita hivyo lazima kuambatane na hatua za “kisheria na kimahakama” za kuuwajibisha utawala huo, na “kuwatambua na kuwafungulia mashitaka makamanda na wahusika wa uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza, kwa lengo la kukomesha miongo mingi ya kutoadhibiwa kwa utawala wa Kizayuni.”
Ikihitimisha taarifa yake, wizara hiyo imeeleza matumaini kwamba, mipango itafanywa kwa ajili ya kuwasilisha mara moja msaada wa kibinadamu kwa raia wa Gaza, na kutangaza utayarifu wa Tehran wa kushiriki katika juhudi hizo za kupeleka misaada katika ukanda huo.